Friday, 20 April 2018

Kwenye ripoti ya CAG hakuna upotevu wa trilioni 1.5 - MagufuliRAIS Dk. John Magufuli amesema katika ripoti aliyopokea kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Assad haikuwa na upotevu wa sh. trilioni 1.5 kama inavyodaiwa.

Rais Magufuli amesema hayo leo wakati akiwaapisha majaji Ikulu Dar es Salaam na kueleza watu wanatumia uhuru wao vibaya kwa kupotosha kitu kilicholeta taharuki.
Rais Magufuli amesema mara baada ya kusikia kuna fedha zilizopotea alipiga simu kwa CAG kuhoji;.
“Mbona kwenye ripoti yako uliyonisomea hapa Ikulu hukunieleza juu wizi wa trilioni 1.5 kwa sababu ungenisomea hapo siku hiyo hiyo ningefukuza watu, kama nimefukuza wakurugenzi watatu siku hiyo kwa kupata hati chafu hawa na trilioni 1.5 uliwaficha wapi nimejaribu kusoma ripoti yako nimeperuzi kila kona sioni mahali zimeandikwa zimepotea trilioni 1.5 na Profesa Assad akaniambia hakuna kitu kama hicho na Katibu Mkuu akasema hakuna trilioni 1.5 iliyoibiwa na serikali,” amesema Rais Magufuli
“Kwa sababu ya uhuru wa mtu kuandika chochote kwenye mitandao kwani hata ndege walisema mbovu hivyo ni kawaida ya uhuru huu, bahati nzuri Controller and Auditor General yupo hapa eti Controller and Auditor General kwenye ripoti yako tumeibiwa trilioni 1.5? Sema hapa hapa watu wajue”
Baada ya kauli hiyo ya Rais Magufuli CAG alisema hakuna kitu kama hicho, pia katibu mkuu alisema hakuna jambo kama hilo na kusisitiza kuwa Hazina wapo vizuri na wapo salama.

No comments:

Post a Comment