Monday, 30 April 2018

Lissu kurejea Tanzania baada ya matibabu

MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anatarajiwa kurejea nyumbani wakati wowote kuanzia sasa. Madaktari nchini Ubelgiji anakopatiwa matibabu wamesema wanamruhusu baada ya kumaliza kumpatia tiba.

Mbunge huyo amekuwa hospitalini tangu Septemba 7, mwaka jana aliposhambuliwa kwa risasi nyumbani kwake Area D, mjini Dodoma. Ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) juzi kuwa kwa sasa hana tena kidonda cha risasi na yupo tayari kurudi nyumbani.

Sina tena kidonda cha risasi, nilipigwa mara 16, sina tena kiungo kilichovunjwa. Nilikuwa nimevunjwa mguu mmoja mara tatu, mikono yote ilikuwa imevunjwa, nilikuwa na risasi nyingi mwilini, na vidonda vingi,” alisema Lissu.

Ameongeza kuwa analazimika kurundi nchini kwa kuwa yeye ni Mbunge, Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri kivuli wa Sheria na Katiba. Alisema kwa majukumu hayo hawezi kwenda mafichoni.

“Siwezi kwenda mafichoni, siwezi kuikimbia nchi yangu, nitarudi Tanzania. Mimi ni mbunge, mimi ni kiongozi bungeni, ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, mimi ni msemaji wa sheria na katiba wa chama changu,” aliongeza Lissu.

Hata hivyo, gazeti Nipashe limemnukuu kaka wa Lissu, wakili Alute Mughwai ambaye anasema kuwa familia yake bado haijapokea taarifa ya siku anayotarajia kurudi.

Alisema familia inachofahamu ni kuwa Lissu amefanyiwa operesheni ya 19 wiki chache zilizopita, hivyo kutakuwa na uangalizi wa afya yake.

No comments:

Post a Comment