Saturday, 14 April 2018

Madai ya kutekelezwa mashambulizi ya kemikali Syria ni hila - Urusi


Sergei Lavrov
WAZIRI wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema ripoti kuhusu shambulio la silaha za kemikali ni njama za washirika wa nje.
Marekani na Ufaransa zimesema zina ushahidi shambulio hilo lilitekelezwa, wakiungana na Uingereza na hivyo wanafikiria kutekeleza mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria.
Urusi, mshirika wa Syria, imeitahadharisha Marekani kuwa mashambulizi ya anga yanaweza kusababisha vita mpya.
Wataalam huria wa masuala ya silaha za kemikali wako njiani kuelekea Ghouta kutafuta ushahidi. Wanatarajiwa kuwasili leo Jumamosi.
Mwito wa kuchukuliwa hatua umekuja baada ya kinachoshukiwa kuwa shambulio la kemikali kutokea mjini Douma Mashariki mwa Ghouta siku ya Jumamosi iliyopita, shambulio lililogharimu maisha ya watu kadhaa, kwa mujibu wa wanaharakati wa upinzani, waokoaji na matabibu.
Mashambulizi ya kemikali yanadaiwa kutokea pia nchini Syria hapo kabla. Mwaka jana, Marekani ilianzisha mashambulizi ya kulipa kisasi moja likielezwa kutokea mjini Khan Sheikhoun.
Serikali ya Rais Bashar Al Assad ambayo inaungwa mkono na Urusi imekana kuhusika na shambulio lolote la kemikali, ikisema ripoti hizo ni za 'kutunga'.
Baada ya majuma sita ya mapambano na vifo vya raia takriban 1,700 Mashariki mwa mji wa Ghouta, serikali ya Sria sasa inadhibiti eneo hilo, lililo nje ya Damascus.
Mchakato wa kuondoa kundi la mwisho la watu 4,000 la wapiganaji wa kiislamu na raia limeendelea jana Ijumaa, kwa mujibu wa waangalizi wa haki za binadamu.

No comments:

Post a Comment