Tuesday, 10 April 2018

Mahakama Uganda yasikiliza kesi dhidi ya ukomo wa umri wa kuwania urais


Rais Yoweri Museveni 
MAHAKAMA ya Kikatiba nchini Uganda inasikiliza kesi iliyoletwa na upande wa upinzani kufuta marekebisho ya Katiba ambayo yanatoa ukomo wa miaka ya kuwania urais wan chi hiyo.
Wabunge waliipigia kura kwa kishindo mwaka uliopita kufuta ukomo wa miaka 75.Ilimaanisha kuwa Rais Yoweri Museveni mwenye miaka 73, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 30, anaweza kuwania tena mwaka 2021.
Mawakili wa upinzani walitoa hoja kuwa marekebisho hayo yaliingizwa "kinyemela" hadi kuwa sheria, na bunge halikufuata kanuni zilizopaswa katika kuweka marekebisho hayo.
Ulinzi umeimarishwa katika eneo la mahakama liliopo katika jiji la Mbale, Mashariki mwa Uganda, na baadhi ya barabara zimefungwa kuepusha machafuko.
Hii ni mara ya kwanza ombi la haki la kikatiba linasikilizwa , anaripoti mwandishi wa BBC Patience Atuhaire kutoka jiji kuu la Kampala.
Miongoni mwa waomba haki ni wabunge wa upande wa upinzani,chama cha wanasheria Uganda na asasi za kiraia.

Upinzani unadai marekebisho hayo hayana msingi kwa sababu yalipitishwa wakati vurugu zilitokea kwenye vipindi ambapo walinzi waliovaa nguo za kawaida waliwatoa wabunge bungeni.
Pia wanatoa hoja kuwa Museveni anataka kuwa rais wa maisha na kuwa mabadiliko hayo yanakiuka misingi ya kidemokrasia, utawala unamilikiwa na watu.
Washirika wa Museveni wanasema marekebisho hayo yanatoa ubaguzi wa kiumri na yalipitishwa baada ya kupata ushauri wa umma.
Chama tawala cha National Resistance Movement kiliongoza mabadiliko hayo kupitia bunge na Rais Museveni akatia saini na kuifanya sheria.
Museveni alishinda awamu ya tano mwaka 2016 katika uchaguzi uliodaiwa kuwa na dosari. Ukomo wa awamu mbili ulifutwa mwaka 2005 ili kumwezesha awanie ofisi tena.

No comments:

Post a Comment