Tuesday, 3 April 2018

Mahakama yamwachia Mbowe na wenzake


WANASIASA saba wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwapatia dhamana wanasiasa sita wiki iliyopita lakini waliendelea kubaki rumande kwa kuwa hawakuwepo mahakamani kukamilisha masharti ya dhamana yao.
Mtuhumiwa wa saba, Halima Mdee, ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, aliongezwa katika orodha ya washtakiwa na kufanya jumla yao kuwa saba.
Wanakabiliwa na mashtaka manane ambayo ni pamoja na kukusanyika na kufanya maandamano kinyume na sheria pamoja na kutoa maneno yanayoweza kusababisha vurugu na chuki miongoni mwa jamii.
Upande wa mashtaka mwanzoni ulihoji kuwa kwa kuwa Halima alikiuka masharti ya dhamana ya polisi na kwamba hakuripoti kituoni kama alivyotakiwa basi anyimwe dhamana kwa kukosa uaminifu.
Lakini hakimu alijibu kwamba, Polisi ni taasisi nyingine na mahakama ni nyingine, hivyo kushindwa kwake kutii dhamana ya polisi hakumuondolei haki ya kupata dhamana ya mahakama.
Kwa msingi huo, Halima Mdee pia amepatiwa dhamana kwa masharti kama yale yale ya wenzake wa awali ambayo ni pamoja na wadhamini wawili, kila mdhamini asaini bondi ya sh. milioni 20 na kukabidhi vitambulisho vinavyotambulika kisheria.
Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi hiyo ameahirisha hadi April 16 kuwa ndio siku ya kusikilizwa kesi ya wanasiasa hao.

No comments:

Post a Comment