Tuesday, 17 April 2018

Makamu wa Rais amwakilisha JPM mkutano wa CHOGM

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini kwenda London, Uingereza kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuia ya Madola (CHOGM), ulioanza jana hadi Aprili 20, mwaka huu (2018).

Samia anamwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika mkutano huo wenye kaulimbiu “Kuelekea Mustakabali wa Pamoja”.

Mkutano huo unaofanyika chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, umefunguliwa na Mkuu wa Jumuia ya Madola, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.

Majadiliano ya Mkutano wa CHOGM 2018 yanajikita kwenye maeneo manne makuu ya kipaumbele ambayo yatajadili namna Jumuia ya Madola inaweza kufikia mustakabali wenye ustawi zaidi, endelevu, wenye haki na usawa zaidi.

Mijadala katika maeneo hayo ya kipaumbele itahusisha masuala mbalimbali ikiwemo, kukuza zaidi biashara na uwekezaji baina ya nchi za Jumuia ya Madola kwa manufaa ya nchi wanachama, kukuza na kuendeleza misingi ya demokrasia, ajenda ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu pamoja na masuala ya uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uhalifu wa kimtandao na usafirishaji wa binadamu.

Jumuia ya Madola ilianzishwa mwaka 1949 kupitia Tamko la London ambalo lilikuwa ni matokeo ya Mkutano wa Mawaziri Wakuu wa nchi za jumuia hiyo yenye wanachama 53 ambapo kati ya hao, nchi 19 ni za Afrika, 7 ni kutoka Asia, 13 ni kutoka nchi za Carribean na mabara ya Amerika, 11 ni kutoka eneo la Pacific na 3 ni kutoka Ulaya.

Ujumbe wa Makamu wa Rais unajumuisha, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka wizara hiyo. Makamu wa Rais na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Aprili 22, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment