Saturday, 28 April 2018

Makonda ‘afunga dirisha’ watoto kutafuta baba zao


Paul Makonda

Peter Simon

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amefunga mchakato wa kutafutia haki watoto waliotelekezwa na baba zao katikamkoa wake.

Makonda amefunga mchakato huo jana Ijumaa ambapo zaidi ya kinababa 2,008 wamekubali kwa maandishi kutoa fedha za matunzo kwa watoto wao huku wengine 2,971 wakiwa wameandikishwa kwa ajili ya kupatiwa Bima ya Afya Bure.

Akitoa tathmini ya mchakato huo jana Makonda amesema tangu kuanza mchakato huo  zaidi ya wananchi 17,000 wamejitokeza kwaajili ya kupata huduma na kati yao 7,184 wamesikilizwa, wengine 10,000 hawakufanikiwa kupata fursa hiyo wakati 270 wamefanikiwa kupimwa DNA.

Kutokana na ukubwa wa tatizo la wazazi kutotekeleza vema majukumu yao, RC Makonda ameunda Kamati ya Wataalamu 15 wakiwemo wanasheria, maofisa ustawi wa jamii, Jeshi la Polisi Dawati la jinsia na asasi za kiraia itakayofanya kazi ya kupitia mapungufu ya kisheria na changamoto zilizojitokeza kisha kutoa mapendekezo kwaajili ya kufikishwa kwa mamlaka husika ili kufanyiwa maboresho ambapo kamati hiyo itaanza kazi Mai 05 chini ya mwenyekiti, wakili Albert Msando.

Aidha, RC Makonda amesema tayari amekabidhi kwa Jeshi la Polisi majina ya kinababa waliokaidi mwito wake ambapo kwa wale walioko mikoani barua zitapelekwa kwa wakuu wa mikoa na waliopo nje ya nchi majina yatafikishwa kwenye ofisi za ubalozi kwa ajili ya utekelezaji.

Hata hivyo,Makonda amesema kupitia mchakato huo amefanikisha watoto wawili wenye asili ya China kupata matunzo hadi watakapokuwa wakubwa chini ya Jumuia ya Watu wa China.

Pamoja na hayo, RC Makonda amewashukuru wanasheria, maofisa ustawi wa jamii, dawati la jinsia, wataalamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa serikali na vyombo vya habari kwa kushirikiana nao bega kwa bega kufanikisha mchakato huo.

No comments:

Post a Comment