Thursday, 19 April 2018

Marufuku kuruka nyumba ya nyasi mnaposambaza umeme- Kalemani


Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani (wa tatu kusho) akizungumza na watendaji wakati akikagua utekelezaji wa mradi wa umeme wa Rea.

Mwandishi Wetu, Tabora

SERIKALI imesema ni marufuku kwa wakandarasi na wataalamu kuruka nyumba wakati wa uunganishaji wa umeme kwa wananchi kupitia Mradi kabambe wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu unaotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

Kauli hiyo ilitolewa wilayani Urambo na Kaliua na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani wakati alipokuwa akikagua utekelezaji wa mchakato wa usambazaji umeme wa Rea katika maeneo hayo.

Amesema ni marufuku kuruka nyumba hata kama ni ya nyasi kama mwananchi anataka umeme na amelipa sh. 27,000 za kuunganishiwa umeme.

Kalemani amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha umeme unafika katika vijiji na vitongoji vyote na kwa wananchi wote bila kubagua.

“Nawaagiza wakandarasi na wataalamu wote hakuna kuruka nyumba wala kubagua nyumba kwa sababu ya kuwa imeezekwa kwa nyasi…umeme ni nyumba kwa nyumba , kaya kwa kaya.., hata kama mtu hajakamilisha nyumba yake kama kuna mti karibu na nyumba yake wekeeni hata hapo ili iwe rahisi kuingiza umeme atakapokuwa amekamilisha nyumba yake” amesisitiza waziri huyo.

Ameongeza kuwa mtindo wa wakandarasi kuchagua nyumba wakati wanapotekekeza majukumu yao ya kuwawekea umeme , na kusema kuwa kwa hivi sasa hilo ni marufku umeme ni kwa wote wanaotaka.

Waziri huyo wa Nishati amefafanua kuwa ni marufuku kuwatoza wananchi wanaotaka kuunganishiwa umeme zaidi ya sh. 27,000 na kutoa mwito kwa mwananchi atayetozwa zaidi ya kiasi hicho atoe taarifa ili hatua kali dhidi ya wahusika zichukuliwe.

Aidha, ametoa mwito kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo ya kuunganishiwa umeme kwa gharama hizo kwani baada ya hapo itabidi walipie kulingana na taratibu za Shirilka la Ugavi wa Umeme Tanzania(Tanesco)

Katika hatua  nyingine Waziri huyo wa Nishati amempongeza Diwani wa Kata ya Vumilia Wilayani Urambo, Kassim Shushu kwa kutoa eneo lake kwa ajili ya kuwapatia Tanesco ili wajenge kituo cha kupozea umeme.

Alisema kitendo hicho cha Diwani wa Kata ya Vumilia kupitia ACT Wazalendo ni cha kizalendo na kimeonesha kuwa maendeleo hayana chama na baada ya kukamilisha mradi Tanesco itabidi ione namna ya kumpa mkono wa shukurani.

No comments:

Post a Comment