Tuesday, 3 April 2018

Maswali 515 kuulizwa mkutano wa 11 wa Bunge


Suleiman Kasei

MKUTANO wa 11 Bunge la 11 umeanza bungeni Dodomaa leo, ambapo pamoja na mjadala wa Bajeti ya 2018/19 maswali 515 yanatarajiwa kuulizwa na wabunge.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Ofisi ya Bunge jana, mkutano huo unatarajiwa kumalizika Juni 29 mwaka 2018.

Taarifa hiyo imesema maswali ya kawaida 515 yataulizwa  na kujibiwa bungeni, aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 38 kanuni ndogo ya (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge wastani wa maswali 72 ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yataulizwa na kujibiwa kwa siku za Alhamisi.

Taarifa hiyo imesema mkutano huo utakuwa ni mahsusi kwa ajili ya mijadala na kupitisha Bajeti ya Serikali pamoja na kujadili Hotuba ya hali ya Uchumi wa Taifa itakayowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango.

Aidha, Bunge litajadili utekelezaji wa bajeti za wizara zote kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 na Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/19.

Shughuli nyingine zitakazofanyika katika mkutano huo ni kiapo cha uaminifu kwa wabunge wawili waliochaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni.

Wabunge walioapishwa ni pamoja na Maulid Mtulia wa jimbo la Kinondoni na Dk. Godwin Mollel wa Siha.

Halikadhalika katika mkutano huu wa Bunge, utafanyika uchaguzi wa wenyeviti watatu wa Bunge kutokana na wenyeviti waliokuwepo kumaliza muda wao kwa Mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.

Vilevile katika mkutano huu Miswada ya Sheria miwili itawasilishwa ambayo ni muswada wa sheria ya fedha za matumizi wa mwaka 2018 na muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2018

Aidha, leo Bunge linatarajia kujadili na kupitisha Azimio la Kuridhia makubaliano ya Paris kuhusu kuboresha utekelezaji wa mkataba wa abadiliko ya Tabianchi.

No comments:

Post a Comment