Friday, 13 April 2018

Mkutano baina ya Moi, Odinga una athari za kisiasa 2022?


Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga (kulia) akipeana mikono na rais mstaafu wa nchi hiyo, Daniel Moi alipokwenda kumjulia hali jana nyumbani kwake baada ya kuwa katika matibabu nje ya taifa kwa muda upatao mwezi mmoja.

ZIARA ya kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya (Nasa), Raila Odinga nyumbani kwa rais wa zamani wa Kenya, Daniel Moi imewaacha wengi vinywa wazi na kuzua mjadala kuhusu uchaguzi wa mwaka 2022 nchini humo.
Mkutano huo unajiri mwezi mmoja baada ya Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kuahidi kufanya kazi pamoja kwa lengo la kuunganisha taifa na wanatarajiwa kuzindua mpango wao katika siku chache zijazo.
Wakati wa ziara hiyo ya jana siku ya Alhamisi, Odinga aliandamana na seneta wa Vihiga George Khaniri na mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir.
Kiongozi huyo wa upinzani alikaribishwa Kabarak na seneta wa Baringo ambaye pia ni mtoto wa Moi, Gidion Moi na katibu mkuu wa chama cha Kanu, Nick Salat.
Hata hivyo, ziara hiyo ilizua hisia kali katika mitandao ya kijamii nchini Kenya huku ikikashifiwa na kuungwa mkono na wengine.

Afya ya Moi
Taarifa iliotumwa katika vyombo vya habari na msaidizi wa Raila Odinga, Dennis Onyango imesema kiongozi huyo wa upinzani alimtembelea kiongozi huyo wa zamani ili kumtakia afya njema baada ya kulazwa hospitalini nchini Israel kwa takriban mwezi mmoja.
Kulingana na taarifa hiyo, Odinga na Moi walidaiwa kuzungumza hali ya kisiasa nchini katika mkutano uliochukua takriban saa moja. Taarifa hiyo ilisema kuwa rais huyo wa zamani alikuwa buheri wa afya.
Inadaiwa kwamba viongozi hao wawili pia walifanya mazungumzo ya kina kuhusu uchaguzi wa 2022 ambao ulimhusisha seneta Moi, kulingana na duru.
Mwana huyo wa mzee Moi kwa sasa anakabiliana kisiasa na makamu wa rais William Ruto ili kudhibiti kura ya bonde la Ufa kabla ya uchaguzi wa 2022 huku wafuasi wa makamu huyo wa rais wakimuona seneta huyo kuwa muharibifu katika kinyang'anyiro hicho.
Na huku uvumi ukisambaa kwamba Odinga alikuwa Kabarak, viongozi kadhaa wanaomuunga mkono Ruto walikashifu hatua hiyo wakidai kuwa mkutano huo ulilenga kumzuia makamu rais kumrithi rais Uhuru Kenyatta.
Odinga ambaye ni mwa wa makamu wa rais wa kwanza nchini Kenya Jaramogi Oginga Odinga alishindwa kwa mara ya nne katika kinyanganyiro cha kuwania urais cha mwaka uliopita.

Raila Odinga
Odinga ni mwanasiasa ambaye huzua hisia kali nchini Kenya- kwa kuwa yeye hupendwa na wengi na vilevile kuchukiwa na wengi. Hakuna mwanasiasa anayezua hisia tofauti kama yeye nchini.
Kwa wafuasi wake ni mpiganiaji wa demokrasia aliyejitolea katika vita dhidi ya udikteta lakini wengine wanamuona kuwa mwanasiasa mwerevu anayejipigania maslahi yake, ambaye yuko tayari kufanya lolote lile ili avune mamlaka.
Aliahirisha harakati zake za kugombea urais 2002, na kumuunga mkono Mwai Kibaki ambaye alimuangusha Uhuru Kenyatta katika uchaguzi uliokifanya chama tawala cha Kanu kupoteza mamlaka kwa mara ya kwanza tangu kenya ijipatie Uhuru 1963.
 Odinga na wafuasi wake wanaamini kwamba alipokonywa ushindi wake katika uchaguzi wa 2007 wakati alipogombea kupitia chama cha ODM dhidi ya Kibaki.
Ni uchaguzi huo uliozua machafuko ya kikabila ambayo yaliosababisha mauaji ya watu 1,300 huku zaidi ya watu wengine 600,000 wakiachwa bila makao.
Itakumbukwa kwamba Raila Odinga aliteswa na kuzuiwa katika mazingira mabaya baada ya mapinduzi ya mwaka 1982 ambayo hayakufanikiwa na utawala wa rais wa zamani Daniel Moi. Lakini kama wanavyosema wanasiasa, siasa hazina uadui wa kudumu.
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment