Tuesday, 10 April 2018

Mkuu wa zamani wa majeshi Sudan Kusini aunda vugu vugu jipya la waasi


Raia wa Sudan Kusini
ALIYEKUWA Mkuu wa Majeshi Sudan Kusini, Paul Malong ameunda vugu vugu jipya la kundi la waasi.
Malong ambaye alitimuliwa katika wadhifa wake na Rais Salva Kiir mwaka jana, amechukua hatua hiyo wakati nchi yake yakianza tena mazungumzo ya amani mjini Addis Abba, Ethiopia.
Mazungumzo hayo pia, yanalenga kufikia makubaliano ya kuachiliwa kwa Makamu wa Rais, Riek Machar ambaye kwa sasa yuko katika kizuizi cha nyumbani nchini Afrika Kusini.
Malong amekuwa akiishutumu serikali kwa rushwa na makosa ya kuifilisi nchi, anasema kundi lake la waasi litakuwa na jukumu kubwa la kuiondoa Sudan Kusini kwenye sintofahamu na kuielekeza katika demokrasia na maendeleo.
Kufuatia kuundwa kwa kundi jipya la waasi, serikali ya Sudan Kusini haijasema neno lolote ambalo linapingana na vikundi kadhaa vya waasi nchini mwake.
Inaarifiwa kuwa wakati Malong alipokuwa ana wadhifa wa mkuu wa majeshi alikuwa akituhumiwa na Umoja wa Mataifa kwa kuratibu mashambulizi ya kikabila dhidi ya raia.
Wakati hayo yakijiri inaarifiwa kuwa mapigano yanaendelea nchini Sudan Kusini baina ya vikosi vya serikali na vikundi vya waasi licha ya mpango wa amani uliosainiwa mwaka 2015.
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment