Sunday, 29 April 2018

MNH kufanikisha mkakati wa upandikizaji figo
Wahudumu wa afya wa hospitali ya Taifa Muhimbili katika picha ya pamoja na wagonjwa wao.


HOSPITALI ya Taifa Muhimbili  (MNH), imeweka mipango ya muda mrefu na mfupi kuhakikisha huduma ya upandikizaji figo inakuwa endelevu na imedhamiria kupandikiza figo kwa wagonjwa zaidi 200 kwa mwaka.

Kauli hiyo imetolewa jana Dare es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha wakati akizungumza na wanahabari baada ya kuruhusiwa wagonjwa wawili ambao wamepandikizwa figo Aprili mwaka huu hospitalini hapo.

Amesema katika  mpango wa muda mfupi, kila mwezi hospitali hiyo itapandikiza figo wagonjwa watano, hivyo kwa mwaka itakuwa imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 60.

“Mipango ya muda mrefu ni kuwa na sehemu maalum ya upandikizaji figo na hivi karibuni MNH itaanza ujenzi wa jengo jipya la ghorofa saba na katika jengo hilo tutatenga sehemu maalum ya upandikizaji figo , kila siku mgonjwa mmoja atapandikizwa figo, kwa wiki tutakuwa tumepandikiza figo wagonjwa watano, kwa mwezi wagonjwa 20 na kwa mwaka tutafanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 240,’’ amesema Aminiel.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Magonjwa ya Figo  Muhimbili , Dk. Jacqueline Shoo amesema tukio hilo ni la kihisoria kwani mwaka jana  hospitali ilifanikiwa kupandikiza figo mgonjwa mmoja na Aprili mwaka huu hospitali hiyo imepandikiza figo wagonjwa wanne kwa mfululizo.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH, Dk. Onesmo Kisanga amesema takribani wagonjwa 800 nchini wanasubiri huduma ya upandikizaji figo na kati ya hao 50 tayari wameandaliwa.

Kwa upande wao wagonjwa waliopandikizwa figo na kuruhusiwa jana Suzana John na Asha Athuman Kisebengo wameishukuru hospitali ya Taifa Muhimbii pamoja na waaalam wake kwa kuwapatia matibabu ya ubingwa wa juu ambayo awali hayakuwepo nchini.

No comments:

Post a Comment