Tuesday, 17 April 2018

Mpina awataka wawekezaji viwanda vya punda kuongeza bei

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye miwani) akikagua kiwanda cha
kuchinja Punda cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo ya mji wa
Dodoma alichokifungua hivi karibuni.

Waziri 
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye miwani) akipata maelezo ya namna ya
kusindika nyama ya punda kutoka kwa mfanyakazi wa wa kiwanda cha 
kuchinja wanyama hao cha Hua Cheng Limited, Elizabeth Peter.

                                       Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (mwenye miwani) akitembezwa katika kiwanda cha
kuchinja Punda cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo mji wa Dodoma alichokifungua hivi karibuni na Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Xun Long Go .(PICHA ZOTE NA JUMANNE MNYAU)
 

John Mapepele, Dodoma

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina 
amewataka wawekezaji wa viwanda vya kuchinja punda nchini kupandisha 
bei ya kununua wanyama hao badala ya sh.200,000 ya sasa kwa 
punda mmoja ili kudhibiti utoroshaji wa mifugo nje ya nchi.

Kauli ya Waziri Mpina imekuja baada kuwepo kwa taarifa kuwa 
zaidi ya punda 10,000 wanatoroshwa mipakani kwa 
siku kwenda nje ya nchi wanakonunuliwa kwa bei ya juu.

Akizungumza 
leo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda cha Punda 
cha Hua Cheng Limited kilichopo nje kidogo ya mji wa Dodoma 
alichokifungua hivi karibuni, Waziri Mpina amesema bei hiyo haiendani 
na gharama halisi ya ufugaji wa punda hali inayowafanya wafugaji
kuwatorosha na hivyo kulikosesha taifa mapato makubwa.

Amesema 
ili punda aweze kufikia hatua ya kuchinjwa inachukua miaka 
miwili ambapo gharama za ufugaji zinakuwa juu ukilinganisha na 
bei anayouzwa kwa wenye viwanda vya punda
nchini.

Aidha, amesema kumekuwa na utoroshwaji mkubwa wa mifugo hao ambapo inakadiriwa
kufikia takribani 1,614,035 kwa mwaka, vitendo hivyo vikifanyika zaidi kwenye mipaka ya
nchi ambapo takribani sh. bilioni 32.28 zinapotea kama ushuru 
na nyingine bilioni 24.21 zikipotea kutokana na kodi ya 
mapato ambayo ingelipwa kwa nyama ambayo ingeuzwa hapo nchini.

Aidha 
Mpina ameunda tume ya wataalam kutoka wizarani kwake ambayo itakuja kufanya 
tathmini kama kiwanda hicho kimetimiza masharti yote 
yaliyotolewa na Serikali baada ya kukifungua Februari Mosi mwaka huu 
ambapo alisema ikibainika kuwa kiwanda hakijakidhi masharti 
yaliyotolewa na Serikali kitachukuliwa hatua kali zaidi za kisheria 
ikiwa ni pamoja na kukifungia kufanya kazi zake.

Aliyataja 
baadhi ya masharti yaliyotolewa na Serikali wakati wa kukifunga kiwanda 
hicho Julai 2017 kuwa ni pamoja na kuwa na ranchi za punda, kuboresha 
kosaafu za punda nchini, kuunda na kuingia mikataba na vikundi vya 
wafugaji wa punda na kuwa na punda wasiopungua 300 katika eneo la 
kuhifadhia mifugo kabla ya kuchinjwa ili kuwahakikisha kwamba 
mifugo wanaangaliwa kwa wiki mbili kabla ya kuchinjwa ili wawe 
katika ubora wa kimataifa.

Waziri Mpina amesema uwekezaji wa 
aina hiyo wa kuongeza thamani ya mazao ya mifugo ni moja ya vipaumbele 
vya wizara yake kwa sasa ili kuchochea kasi ya kufanikisha azma ya
Tanzania ya viwanda.

Aidha, amewahakikishia wawekezaji wa 
kiwanda hicho kuwa endapo watakuwa wamekamilisha masharti atawapa kibali 
cha kudumu ambapo pia atawaongezea idadi ya kuchinja punda kutoka
20 wa sasa ili vijana wengi wapate ajira na kiwanda kiweze 
kuchangia zaidi katika mapato ya Serikali.

Mpina amewahimiza 
wawekezaji hao kuhakikisha wanawasaidia wafugaji katika kuongeza
uzalishaji, kupambana na maradhi, upatikanaji wa maji na malisho kwa 
mifugo.

Amesema idadi ya punda waliopo nchini ni 520,000 tu hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuongeza uzalishaji.

Naye 
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Xun Long Go ameshukuru Waziri Mpina 
kwa kufungua kiwanda hicho ambapo amesema hadi sasa 
kimezalisha na kuuza tani 224 za nyama ya punda kwenda nchini China 
na Vietinam ambapo pia tani 52 za ngozi ya punda ilizalishwa na kuuzwa k
uanzi Februari, mwaka huu (2018).

Alisema kiwanda hicho kimeajiri watanzania 55 ambapo hadi sasa kina punda 88 katika maeneo ya Chalinze na Zuzu mkoani Dodoma.

Kaimu 
Mkurugenzi wa Uzalishaji Mifugo na Masoko wa Wizara ya Mifugo na 
Uvuvi, Lucia Chacha ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kubuni 
mbinu za kuwasaidia wafugaji kwa kuwapatia elimu bora zaidi ya ufufaji 
wa punda ili waweze kuwazalisha kwa wingi zaidi kuliko ilivyo sasa

Hadi 
sasa Tanzania ina viwanda viwili tu vya kuchinja na kuuza nyama ya 
punda ambavyo ni kiwanda cha Punda cha Huacheng Limited kilichopo nje 
kidogo ya mji wa Dodoma na cha Fang Hua kilichopo Shinyanga 
ambavyo vyote vimepewa kibali cha kuchinja Punda 20 kwa siku kila 
kimoja.

No comments:

Post a Comment