Monday, 30 April 2018

Mti alioupanda Macron ikulu ya Whitehouse wapotea


MTI ambao Rais Donald Trump alipewa kama zawadi na rais mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron umetoweka kutoka kwenye bustani ya ikulu ya White House Marekani.
Viongozi hao wawili waliupanda mti huo, uliotoka eneo lililoshuhudia vita vya dunia vya kwanza Kaskazini Mashariki mwa Ufaransa, wiki iliyopita.
Macron amesema mti huo utakuwa ukumbusho wa 'uhusiano unaotuunganisha'.
Lakini mpiga picha wa shirika la habari la Uingereza Reuters juzi Jumamosi alipiga picha ya nyasi chache za njano tu zilizosalia katika eneo ambako mti huo ulipandwa.
Baadaye balozi wa Ufaransa nchini Marekani alituma ujumbe katika Twitter kwamba mti huo umewekwa kwenye karantini. Mti huo unatoka eneo ambako kulishuhudiwa vita vya kwanza vya dunia mwaka 1918.
Takriban wanajeshi 2,000 wa Marekani walifariki katika vita hivyo Kaskazini Mashariki mwa mji mkuu Paris.
Hata hivyo, siku nne baada ya kupandwa, mti umepotea. Kukiwa hakuna sababu rasmi iliotolewa kwa kupotea mti huo, kumekuwa na uvumi katika mtandao kuhusu hatma ya mti huo.
Radio ya Ufaransa Franceinfo inanukuu mtandao wa upaliliaji bustani gerbaud.com, unaosema kwamba aina hii ya mti huwa ni vizuri ukipandwa wakati wa msimu wa mapukutiko, ili kutoa nafasi mizizi ijikite na kukuwa vizuri, kuweza 'kukabiliana na joto kali la msimu unaofuata wa joto'.
"Huenda mti huo ukapandwa upya mwezi Oktoba," Franceinfo inakisia. Baadaye balozi wa Ufaransa Gerard Araud alisema mti huo umewekwa kwenye karantini.
Araud pia alijaribu kuondoa wasiwasi kuhusu iwapo mti huo kweli ulipandwa.
Mtandao wa idara ya ushuru na ulinzi wa mipakani Marekani umeeleza kuwa miti inayotoka nchi za nje , inayonuiwa kupandwa inahitaji vibali maalum kabla ya kuletwa nchini.

No comments:

Post a Comment