Saturday, 14 April 2018

Mwakyembe awafunda watumishi wa wizara yake


Dk. Harrison Mwakyembe (aliyesimama)
Mwandishi Wetu, Dodoma
WATUMISHI wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wamehimizwa kutumia muda wao wa kazi kuwahudumia wananchi kwa kujibu hoja na kutatua kero zao kwa haraka na ufanisi.
Agizo hilo limetolewa mkoani Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Dk. Harisson Mwakyembe alipokuwa akifungua kikao cha 13 cha Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo, ambacho hufanyika mara mbili kwa mwaka ili kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za watumishi.
“Ni wajibu wa kila mtumishi kuzingatia maadili na weledi katika kuhakikisha utumishi wa umma unaheshimika na kuwajibika kwa wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa kazi zetu” amesema Dk. Mwakyembe.
Aidha, ameziagiza mamlaka zinazosimamia nidhamu katika wizara hiyo kutosita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wasiotimiza wajibu wao ili kuimarisha utendaji wa kazi.
“Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli, ipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha taratibu za kiutendaji zinafuatwa na kuzingatiwa” amebainisha.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Susan Mlawi amemshukuru Waziri Dk. Mwakyembe kwa kuwafungulia kikao hicho ambacho kipo kwa mujibu wa sheria, na kuwasisitiza watumishi kuyafanyia kazi yale yote waliyoelezwa.
“Nawaomba watumishi kuzingatia na kutekeleza wajibu wenu katika majukumu yenu ya kila siku kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizoainishwa katika mikataba ya ajira” amesema Susan.
Naye Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Makoye Nkenyenge alimshukuru mgeni rasmi kwa niaba ya wajumbe wote na kuahidi kuyafanyia kazi yale yote aliyoyaeleza ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment