Wednesday, 4 April 2018

Mwanri awa mgeni rasmi kongamano la utunzaji misitu

Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi

MKUU wa mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri amekuwa mgeni rasmi katika kongamano la utunzaji wa misitu litakaloambatana na maadhimisho ya upandaji miti kitaifa wilayani Kishapu.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu,  Nyabaganga Taraba amesema kongamano hilo linafanyika leo ambapo wageni mbalimbali wameshiriki.

Taraba ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo amesema washiriki wanapatiwa elimu kupitia mada mbalimbali kuhusu misitu inayotolewa na watoa mada kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Miongoni mwa washiriki hao ni pamoja na viongozi wa wilaya na halmashauri zote za mkoa wa Shinyanga, wataalamu wa misitu nchini, wataalamu kutoka halmashauri mbalimbali na wananchi.

Wananchi wengi wameshiriki kupatiwa elimu kuhusu umuhimu wa utunzaji miti katika siku tatu za maadhimisho hayo yaliyoanza jana na kufikia tamati kesho kwenye viwanja vya Shirecu wilayani Kishapu.

Amesema maadhimisho hayo yanaambatana na maonesho ya bidhaa za misitu pamoja na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali.

Katika kilele cha maadhimisho hayo hapo kesho, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla. Kauli mbiu ni ‘Tanzania ya Viwanda inawezekana, panda miti kwa maendeleo ya Viwanda.

Shughuli za upandaji miti zimefanyika katika kila kaya ambapo kila moja imekabidhiwa miche kwa ajili ya kuipanda katika maeneo yao na kutakiwa kuitunza.

Upandaji miti unafanyika katika vijiji vya Mwatuju na Songwa ambapo lengo ni kuifanya wilaya ya Kishapu kuwa ya kijani kwa kuondoa hali ya jangwa inayoinyemelea.

No comments:

Post a Comment