Monday, 9 April 2018

Naipongeza Serikali kwa kuwarudisha kazini wafanyakazi iliyowaondoa - Mandai


Mkurugenzi wa Kampuni za Mandai, Abdallah Mandai.

Claudia Kayombo

MKURUGENZI wa Kampuni za Mandai (Mandai group of Co.), Abdallah Mandai amepongeza hatua ya serikali ya kuwarudisha kazini wafanyakazi iliyowaondoa kwa kuwa na vyeti vya elimu ya msingi.

Akizungumza Dar es Salaam leo, amesema hana shaka kuwa hizo ni jitihada za serikali ya Awamu ya Tano za kuhakikisha kuwa wananchi wake wanaishi maisha bora.

“Naipongeza sana serikali kutokana na hatua hiyo ya kuwarudisha kazini wafanyakazi wote ambao waliondolewa kutokana na kuwa na elimu ya darasa la saba, sina shaka kuwa Rais Dk. John Magufuli ameona ni haki yao kuendelea na kazi hadi watakapostaafu,”amesema mkurugenzi huyo.

Ameongeza kuwa hana shaka kuwa hatua hiyo ya serikali imepokelewa kwa furaha na wengi wakiwemo walioondolewa kazini, familia zao, ndugu jamaa na marafiki.

Amebainisha kuwa Rais Magufuli katika maeneo mengi amejipambanua kujali hali duni za wananchi wake na kwamba hana shaka kuwa hata hili amelifanya kutokana na huruma aliyonayo kwa wananchi wake.

Aidha, amewataka wanaorudi kazini kufanya kazi kwa weredi na umakini mkubwa ili serikali iliyowarudisha kazini ione jitihada zao, kwa kuwa uzoefu unaonesha kuwa watu wenye elimu ya chini ni wachapazi wazuri kuliko pengine wale wenye digrii.

Leo bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Utumishi, George Mkuchika ametangaza kurudishwa kazi waajiriwa wote waliondolewa kazini kwa kuwa na vyeti vya elimu ya msingi na kuagiza kulipwa mishahara yao yote.

No comments:

Post a Comment