Thursday, 19 April 2018

Nitajiondoa wakati wa mazungumzo na Kim iwapo hayataonesha kuzaa matunda - Trump


Donald Trump
RAIS wa Marekani, Donald Trump anasema iwapo mazungumzo yake na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un hayazai matunda 'atainuka na kuondoka katika mazungumzo hayo'.
Katika mkutano wa pamoja na vyombo vya habari, yeye na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe walisema shinikizo dhidi ya Korea Kaskazini ni sharti iendelee kwa kukataa kusitisha utengezaji wa silaha za nyuklia.
Abe yuko katika mgahawa wa Rais Trump wa Mar-a-Lago resort mjini Florida kwa mazungumzo. Mapema Trump alithibitisha kwamba mkurugenzi wa CIA Mike Pompeo alifanya ziara ya kisiri hadi Korea Kaskazini ili kukutana na Kim Jong Un.
Amesema kuwa Pompeo aliweka uhusiano mzuri na Kim ambaye Trump alimuita 'mtu mdogo' na kwamba mkutano wao ulifanyika vizuri. Ziara hiyo iliadhimisha mawasiliano ya juu kati ya Marekani na Korea Kaskazini tangu mwaka 2000.
Mkutano huo kati ya Trump na Kim unatarajiwa kufanyika kufikia mwezi Juni. Maelezo ikiwemo eneo litakaloandaa mkutano huo bado yanaendelea kufanyiwa kazi.
Rais Trump amesema katika mkutano wa pamoja kwamba iwapo anadhani kwamba mkutano huo hautafanikiwa basi hatoshiriki na kwamba iwapo mkutano huo umefanyika na haoni matunda yake basi atasimama na kuondoka.
''Kampeni yetu ya shinikizo itaendelea hadi pale Korea Kaskazini itakapositisha utengezaji wa silaha za Kinyuklia'', aliongezea.
"Kama nilivyosema awali nyota ya Korea Kaskazini itang'aa wakati taifa hilo litakaposimamisha mpango wake wa kinyuklia .Itakuwa siku kuu kwao na itakuwa siku kuu ulimwenguni.
"Kuhusu biashara, viongozi hao wawili walikubaliana kuanza mazungumzo kuhusu biashara huru na isiyopendelea upande wowote.
Trump amesema Marekani itaendelea kupinga hatua ya kujiunga na biashara ya ushirikiano ya Trans Pacific Partnership hadi pale Japan na washirika wengine watakapoweka makubaliano ambayo Marekani haiwezi kukataa.
Marekani hata hivyo haikuiondoa Japan katika kuitoza kodi ya vyuma na alminium kama alivyowafanyia washirika wengine wa Marekani.
Akizungumzia kuhusu Korea Kaskazini Abe amemtaka Rais Trump kusaidia kuachiliwa huru kwa raia wa Japan waliotekwa nyara na Korea Kaskazini miaka ya 1970 na 1980.
Korea Kaskazini imekiri kuwateka nyara raia 13 wa Japan ili kuwatumia kuwafunza wapelelezi wake kuhusu forodha ya Japan. Japan inaamini takwimu hizo ziko juu.
Suala hilo limeathiri pakubwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili kwa miongo kadhaa. Raia watatu wa Marekani pia wanazuiliwa nchini Korea Kaskazini.
Trump anasema Marekani itatumia kila njia ili kuhakikisha kuwa raia wa taifa hilo waliotekwa nyara na Japan wanarudishwa nyumbani.

No comments:

Post a Comment