Sunday, 29 April 2018

Njia za kuepuka, kukabili tatizo la saratani ya mapafu


Claudia Kayombo
SARATANI ya mapafu inatajwa na watafiti kuwa ni miongoni mwa saratani hatari zaidi duniani.
Hata hivyo, ni moja sarani ambazo zinazuilika iwapo jamii itapewa elimu ya namna ya kuepukana nayo ukilinganisha na aina nyingine karibu 200 za maradhi hayo.
Wataalamu wa tiba ya maradhi ya saratani wanasema kuacha uvutaji wa mazao ya tumbaku kunamweka mtu katika uwezekano mkubwa wa kujiepusha si tu na aina hii ya saratani bali hata na nyingine nyingi zinazosababishwa na tumbaku.
Hata hivyo, saratani ya mapafu haiepukwi tu kwa kuacha kuvuta moshi wa tumbaku hata ule utokanao na dizeli kutoka kwenye magari, ule wa viwandani, na hata wa shughuli za mapishi.
Aina hii ya saratani ni tishio kwa sababu inaua kama zilivyo aina nyingine, hivyo ni vema jamii izingatie maelezo ya wataalamu kuwa ili kuepukana nao ni vema kuacha kuvuta moshi wowote au kukaa maeneo yenye moshi daima.
Kulingana na taasisi ya utafiti ya saratani ya Umoja wa Ulaya, ni kwamba aina nne za saratani zinazotatiza watu wengi ni ya mapafu, ya titi, utumbo na tezi dume.
Taasisi hiyo inafafanua kuwa zaidi ya visa vinne kati ya 10 vya saratani  duniani kote, aina hizi zinasababisha asilimia 42 kwa mujibu wa mradi wa Globocan.
Mradi wa Globocan ni hazina data ya habari kuhusu saratani ambayo husimamiwa na Chama cha Kimataifa cha Sajili za Saratani.
Saratani ya mapafu ndiyo inayopatikana sana miongoni mwa wanaume, huku saratani ya matiti ikipatikana zaidi miongoni mwa wanawake.
Saratani si ugonjwa mmoja, ni magonjwa zaidi ya 200, kila ugonjwa ukiwa na dalili zake tofauti na njia za kuupata na pia kuutibu.
Shirika la Afya Duniani linasema visa vya kansa vitaongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Aidha, uchunguzi unaonesha kuwa uvutaji sigara hapa nchini ni huru mno ukilinganisha na hali ilivyo katika mataifa mengine ikiwemo nchi jirani ya Kenya, hali ambayo inaiweka jamii kubwa katika hatari ya kukumbwa na maradhi ya saratani.
Watu wengi hapa nchini wamekuwa wakivuta sigara hadharani tena kwenye mikusanyiko ya watu kama vile kwenye vituo vya daladala na kumbi za starehe jambo ambalo ni hatari kwa wasiovuta pia.
Katika nchi ya Kenya kuna sheria zinazoandamana na kanuni zinazopinga watu kuvuta sigara hadharani hususan kwenye mikusanyiko ya watu. Sheria hizo zinalenga kulinda afya za wananchi wao.
Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Kudhibiti Tumbaku Tanzania (TTCF), Dk. Lutgard Kagaruki anasema kuna haja ya kudhibiti matumizi ya tumbaku nchini kwa kupiga marufuku matangazo, promosheni na ufadhili wa zao hilo.
“Katika hili mwendelezo wa matangazo, promosheni na ufadhili wa bidhaa za tumbaku hapa nchini umesababisha ongezeko kubwa la matumizi ya tumbaku miongoni mwa vijana,” anasema.
Anabainisha kuwa hilo ni kulingana na utafiti uliofanywa mwaka 2008 na Global Youth Tobacco Survey na kubaini kuwa asilimia 10.6 ya wanafunzi nchini wanatumia bidhaa zitokanazo na tumbaku.
“Kutokana na hilo, ndiyo maana Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), limeona athari hizo na kuamua Mei 31 iwe maadhimisho ya Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani na kuielimisha jamii kuhusu madhara yake kiafya,” anasema mkurugenzi huyo.
Hali kadhalika anasema utafiti mwingine uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwaka 2010 ulionesha kuwa zaidi ya asilimia 32 ya saratani zote wagonjwa wa saratani waliowatibu kilichosababisha ni  matumizi ya tumbaku.
Kumtibu mgonjwa mmoja wa saratani ya mapafu serikali inatumia dola za Marekani milioni 40 sawa na shilingi trilioni 6.4 anasema.
Licha ya saratani ya mapafu, Kagaruki anataja magonjwa mengine yanayosababishwa na tumbaku kuwa ni pamoja na maradhi ya moyo, upungufu wa nguvu za kiume, vidonda vya tumbo, kisukari na kifua sugu.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kupinga matumizi ya tumbaku, Mei 31 mwaka jana, Dk. Kagaruki anasema chama chake kimekuwa kikisisitiza umuhimu wa kulima mazao mbadala wa tumbaku kama ufuta, karanga na alizeti.
“Siyo hivyo tu sisi tumekuwa tukipinga kuwepo utaratibu wa kutenga maeneo ya kuvutia sigara kama ambavyo baadhi ya nchi zimekuwa zikifanya hivyo kwa sababu kuwatengea maeneo wavutaji ni sawa na kuwaruhusu wakajiue,” anasema Dk. Kagaruki.
Si hivyo tu anasema ripoti ya WHO kuhusu madhara ya tumbaku inaonesha kuwa katika kila sekunde nane mtu mmoja anafariki dunia kutokana na madhara yanayosababishwa na uvutaji wa bidhaa za tumbaku.
Pia watu wazima saba miongoni mwa 10 wanaovuta walianza kufanya hivyo wakiwa na umri mdogo na hivyo kuwa katika hatari ya kuishi maisha mafupi ambayo ni miaka 20 hadi 25 waliyotakiwa kuishi zaidi.
Anasema ripoti ya WHO inaonesha kuwa katika karne moja iliyopita zaidi ya watu milioni 100 walifariki dunia kutokana na uvutaji wa sigara na takwimu nyingine zinaonesha kuwa watu zaidi ya milioni sita, wanafariki dunia kila mwaka kutokana na uvutaji wa bidhaa zinazotokana na tumbaku.
Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubya akizungumza wakati wa mkutano wa wadau kutoka mataifa mbalimbali duniani uliofanyika mwaka jana wenye lengo la kuwakwamua wananchi kuondokana na ukulima wa zao la tumbaku na kutafuta kipato kwa njia nyingine, anasema wakulima wa zao hilo hupata madhara sawa na watumiaji.
Hata hivyo anakiri kuwa serikali inafahamu kuwa takwimu zinaonesha hasara inayopatikana kutokana na zao hilo ni mara mbili ya faida inayopatikana.

No comments:

Post a Comment