Friday, 20 April 2018

Rais Trump hashauriki - Comey

ALIYEKUWA mkuu wa FBI nchini Marekani, James Comey ameiambia BBC kuwa haamini kuna kiongozi yoyote wa karibu na Rais wa Marekani Donald Trump anaweza kumbadilisha tabia yake.
Anasema tabia zake zinahatarisha hadhi ya nchi. Kabla ya kufukuzwa na Trump, Comey aliongoza uchunguzi dhidi ya kuhusika kwa Urusi katika uchaguzi wa Marekani.
Akizungumza katika kipindi cha Newsnight Comey anasema tabia za Trump zinaathiri wale wanaomzunguka.

James Comey 
"Nadhani tabia yake inaathiri hasa hasa kwenye suala la ukweli na jambo la msingi ni jinsi tabia hizo zinavyoathiri taasisi na watu wa karibu yake. Ana tabia ya kuongea uongo na kuwa lazimisha wale wanamuunga mkono kukubalina naye na kuamini," anasema Comey
Trump alimshutumu Comey kuwa anayoyazungumza na uongo na siasa zake za ubaguzi.
Hadithi hii inaanzia wakati wa uchaguzi wa urais mwaka 2016, wakati Comey alikuwa mkurugenzi wa FBI, na uchunguzi kuhusu namna mgombea wa urais wa chama cha Democrat Hillary Clinton alivyozishughulikia barua pepe za siri katika kompyuta binafsi wakati akiwa waziri wa mambo ya nje.
Mnamo Julai 2016, Comey alisema kwamba hakuwa na umakini katika namna alivyozishughulikia barua pepe hizo, lakini FBI haitomshtaki.
Hata hivyo ,Oktoba siku kadhaa kabla ya uchaguzi, alituma barua bungeni akiliarifu kwamba FBI linaanzisha upya uchunguzi baada ya kugundua barua pepe zaidi.
Barua hiyo ilifichuliwa kwa umma - na Hillary Clinton akasema hatua hiyo ndiyo iliyompa Trump ushindi.
Mnamo Novemba, FBI ilisema imekamilisha ukaguzi wa barua pepe hizo mpya zilizogunduliwa na kwa mara nyingine likasema halitomshtaki.
Trump alipopata urais, Comey alisema kuwa alijaribu kumshurutisha aape kumtii - Jambo ambalo rais analikana pakubwa.
Machi 2017, wakati uchunguzi ulipokuwa unafanywa na FBI kuhusu tuhuma za ushirikiano kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi inatuhumiwa kwamba Trump alimshinikiza Comey kutangaza wazi kwamba rais hatochunguzwa kibinafsi - jambo ambalo mkurugenzi huyo wa zamani wa FBI alikataa kufanya hivyo.
Baadhi ya wanasiasa wa Democrats walimlaumu Comey kwa kumfanya Clinton apoteze kura katika uchaguzi huo, huku wafuasi wa Trump walihisi kwamba anamlenga rais katika uchunguzi huo.
Alifutwa kazi na rais Trump mwezi Mei, na alipata taarifa kuhusu kutimuliwa kwake katika vyombo vya habari nchini humo.
Comey alihojiwa bungeni kuhusu uchunguzi huo wa uwezekano wa kuwepo uhusiano kati ya kampeni ya Trump na Urusi na kutimuliwa kwake, na alimtuhumu rais kwa kusema uongo na kumchafulia jina.
Rais wa Marekani Donald Trump.

No comments:

Post a Comment