Tuesday, 17 April 2018

Saba wahofiwa kufariki dunia kwa mafuriko Dar es SalaamNyumba zilizozingirwa na maji baada ya mvua kubwa jijini Dar es Salaam.

Peter Simon


WATU Saba wanahofiwa kufariki dunia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alithibitisha kutokea vifo Saba hapo jana na kueleza kwamba miongoni mwa miili hiyo mmoja ulikutwa ukielea maeneo ya Jangwani.

Sanjari na hilo Kamanda Mambosasa amesema maeneo mengi jijini Dar es Salaam yamejaa maji, na kuwataka watu kuwa makini wanapotumia barabara hasa sehemu zenye makorongo, na kuwaangalia zaidi watoto ambao wanapita mara kwa mara wakienda shule au wakiwa wanarudi kutoka shule au maeneo mengine.

“Watu wasijaribu maji, ukijaribu maji ujue utaondoka nayo, kwa hiyo watoto wetu wanapokwenda shuleni tuwasindikize, sehemu nyingi zenye makorongo kwa mfano kule Kinyerezi, kule Goba kule Makongo, zile shortcut zote maji yamejaa, watu wajiepushe kutumia njia hizo, watapoteza watoto wakiwa wanaenda au kutoka shule”, amesisitiza Kamanda Mambosasa.

Jeshi la Polisi limesema litaendelea kutoa taarifa za sehemu mbali mbali kuhusu hali ya mvua, ambayo inaendelea kuathiri sehemu kubwa ya nchi.

No comments:

Post a Comment