Saturday, 28 April 2018

Sababu saba Emirates kutua JNIA


Emirates ya Airbus A380 

Suleiman Kasei

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCCA), imetaja sababu saba zilizosababisha ndege ya Shirika la Ndege la Emirates aina ya Airbus A380 kutua katika Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).

Sababu hizo zimetajwa na Mkurugenzi wa TCCA, Hamza Johari wakati akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa ujio wa ndege hiyo umeitangaza Tanzania kimataifa.

Johari ametaja sababu hizo kuwa ni eneo la kukimbilia ndege wakati wa kutua au kupaa ambapo uwanja wa JNIA una urefu wa kilomita 3.1 na ndege hiyo ilihitaji kilomita 3 ili kutua na upana mita 60 hadi 75 ambapo JNIA ikiwa na upana wa mita 60.

Amesema pia ipo mifumo mbalimbali yakitaalam. kama kushuka katika kona stahiki, njia ya kutembelea na mifumo  kama DME, VOR na mingine muhimu ambayo ipo.

“Pia sababu nyingine ni vifaa vya kuzima moto iwapo kuna dharura ya moto itaweza kuzimwa na Airbus A380 inahitaji mfumo wa kuzima wa fungu la tisa ambapo Tanzania inavigezo, kwani katika oparesheni za ndege kutua na kupaa ni vitu muhimu,” amesema.

Amesema sababu nyingine ni huduma za ardhini,ambazo zinatolewa baada ya ndege kutua kama kuwasha, kusukuma, uwepo wa mafuta ya uhakika na kushusha abiria na mizigo.

Johari ametaja sababu nyingine ni hali ya usalama ambapo kwa Tanzania sasa ipo asilimia 64.3 kutokana 37.8, ufanyaji kazi wa hudumu wote wa uwanja na usafiri pale ambapo inahitajika.

Amesema ndege hiyo ambayo ilibeba abiria 476 na wafanyakazi 27 walihudumia katika kiwango cha kimataifa pamoja na muda wa saa saba unakuwa na wingi wa ndege.

“Saa saba ni muda ambao tunapokea ndege nyingi hivyo abiria wanakuwa wengi kwa siku ile tulihudumia zaidi ya abiria 2,000 jambo ambalo sio rahisi hasa ukiwa hujajipanga,” amesema.

Amebainisha kuwa abiria wa ndege hiyo na wafanyakazi walilala katika hoteli za nyota tano na nne, kupatiwa viza na huduma nyingine ambazo zote kwa pamoja zimeingizia nchi fedha nyingi.

Johari amesema pia ujio wa ndege hiyo kubwa duniani ulikumbana na changamoto ya ukosefu wa ngazi ya kushusha abiria katika ghorofa ya pili na kujipanga hasa iwapo itakuja kwa muda wa mchana ambao kuna abiria wengi.

Aidha, mkurugenzi huyo amesema pia wamejitangaza kimataifa kuwa wapo tayari kuhudumia ndege yoyote.

Pia amesema ujio wa ndege hiyo kubwa duniani umewawezesha kujiamini na kujenga uaminifu kwa wadau wa biashara ya usafiri wa anga.

Kwa upande mwingine, Johari amesema amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Afrika la Huduma za Anga na Uongozaji Ndege jambo ambalo litasaidia asimamie sera na mipango ya Tanzania na nchi za Afrika kwa ujumla.

Pia amesema Tanzania inataraja kumpokea Rais wa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), Dk. Olomuyiwa Benard Aliu kukabidhi tuzo ya heshima ya Rais wa shirika hilo baada ya kupata alama 64.3 kutoka 37.8 ya zamani.

No comments:

Post a Comment