Wednesday, 4 April 2018

Samia aridhishwa viongozi CCM kurudi kwa wananchiMjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Samia Suluhu Hassan akiwasikiliza wananchi katika hafla ya maandalizi ya kilimo cha mpunga na upandaji wa mpunga katika bonde la kizimbani Unguja, kilimo kinaendeshwa na wana- CCM wa jimbo la Bububu na maeneo jirani.


Mwandishi Wetu, Zanzibar


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameridhishwa na kasi ya viongozi wa chama hicho wa kurejesha utamaduni wa kurudi kwa wananchi wa chini kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Amesema kwa kiasi kikubwa wananchi walikuwa wamepoteza imani kwa CCM kutokana na kuwa viongozi wengi walikuwa wanatabia ya kukaa ofisini n kutowafikia wananchi hao kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wananchi wanaotumia bonde la mpunga la Kizimbani Unguja katika ziara yake ya kutembelea miradi mbali mbali inayotekelezwa na  wana- CCM katika maeneo hayo ya kilimo cha mpunga.

 Samia ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  amesema ile dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya imeanza kustawi katika fikra za Wana- CCM na kufanyiwa kazi kupitia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020/2015.

“CCM mpya imeanza kuonekana ikiwemo kuwafuatilia wananchi wa chini zaidi kwa mfano katika mikakati ya kufuatilia kaya maskini kwenye miradi ya Tasaf viongozi wa chama wameanza kuonekana kufuatilia utatuzi wa changamoto za kuondoa hali ya umaskini hivyo CCM iko karibu na wananchi kwa sasa,” amesema Samia.

Katika maelezo yake Makamu huyo wa Rais, amesema ni ukweli kuwa chama cha siasa ni watu na kwamba chama chochote kinapaswa kuwa karibu na wananchi  kwani wao ndio walioiweka Serikali madarakani.

Amewataka viongozi na watendaji wa CCM kukukumbushana kuwa pindi wanapopewa dhamana za uongozi hawatakiwi kukaa ofisini bali wana majukumu yao ya msingi ni kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia, amewapongeza wanajumuia na wakulima wa kilimo cha mpunga Kizimbani kwa juhudi zao za kuungana katika jumuia ambapo itawawezesha kusaidiwa kwa urahisi kwa kuwa wapo pamoja kwenye sekta ya kilimo.
Makamu wa Rais Samia ameahidi kuwasaidia fedha na kuwapatia trekta kupitia CCM ili liwasaidie katika kilimo chao cha mpunga kwenye mabonde hayo ya mpunga ya Kizimbani na maeneo mengine.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Dk.Abdulla  Juma  Mabodi  amesema CCM inaendelea kutatua  kero za wananchi hatua kwa hatua na kwa sasa imesaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wanaolima zao la mpunga katika bonde la Kizimbani.

Dk. Mabodi amesema lengo ni kuwasaidia wakulima hao ni kukabiliana na changamoto za upungufu wa chakula hasa mchele ambao wakulima wengi wamewekeza nguvu zao katika kilimo cha mpunga.

Mapema Mbunge wa Jimbo la Bububu Mwatantakaje Haji Juma amesema bonde hilo lina wakulima zaidi ya 700 kutoka jimbo hilo na maeneo jirani.

Amesema mradi wa kilimo cha mpunga katika bonde hilo ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, ambapo viongozi mbali mbali wa jimbo wamekuwa wakitumia rasilimali fedha kuunga mkono juhudi za wananchi ambao ni wakulima wa zao la mpunga.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan akifungua Tawi la CCM Fuoni Kibondeni lililojengwa na wana-CCM  kwa kushirikiana na viongozi mbali mbali wa chama hicho.

No comments:

Post a Comment