Friday, 20 April 2018

Saratani ya titi inavyoweka hatarini maisha ya wanawake wengi


Waziri wa Afya. Ummy Mwalimu

Claudia Kayombo

UGONJWA wa saratani ya matiti umekuwa tishio kwa wanawake katika mataifa mengi yanayoendelea kwa kuwa takwimu za waathirika zimekuwa zikiongezeka badala ya kupungua.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema viashiria vya saratani vitaongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga katika Taasisi ya Ocean Road, Dk. Chrispin Kahesa, anasema tofauti na magonjwa mengine yamekuwa yakionesha dalili mapema saratani ya matiti dalili zake si za mapema.

Anasema aina hii ya saratani inaweka hatarini maisha ya wanawake wengi kwani ndiyo waathirika wakubwa wa tatizo hilo ukilinganisha na wanaume.

Daktari huyo anasema hadi sasa hakuna sababu ya moja kwa moja inayosababisha saratani hiyo na kwamba wanasayansi wanaendelea kutafuta chanzo.

Hata hivyo, anasema yapo mambo ambayo yanaaminika kuchangia tatizo hilo ikiwemo aina fulani ya chembe ya urithi inayosababisha nyingine zipoteze ufanisi wake.

Kuanza hedhi katika umri mdogo au kukoma katika umri mkubwa, kutozaa kabisa na kutonyonyesha kabisa au kunyonyesha kwa muda mfupi vinaweza kuwa sababu ya ugonjwa huo.

Pia matumizi ya mafuta mengi katika vyakula, kutofanya mazoezi mara kwa mara, unene kupita kiasi, uvutaji sigara, utumiaji pombe kupita kiasi na historia ya saratani ya matiti katika familia ni sababu nyingine ya maradhi hayo.

Aidha, anasema saratani hii inawapata pia wanaume ambapo si kwa kiwango kikubwa kwani hadi sasa hapa nchini ni asilimia moja tu ya wanaume ndiyo wamegundulika kukumbwa na tatizo hilo.

Dk. Mark Mseti mkuu wa kitengo cha Bima katika taasisi hiyo anasema matibabu ya saratani yanategemea vitu vikubwa vitatu, ambavyo ni kufahamu hatua ya saratani ilipofikia, hali ya ugonjwa na ridhaa ya mgonjwa kuhusu aina ya matibabu anayotaka kupatiwa.

“Hapa cha msingi ni muhimu kuwa maradhi ya saratani hayaambukizi na yanaweza kukaa katika mwili wa mtu kati miaka mitano hadi 10 ndipo dalili zake huanza kujitokeza wazi,”anasema Dk. Mseti.

Anatoa mwito kwa jamii kujitokeza kufanyiwa uchunguzi hospitalini mara kwa mara ili kama maradhi hayo yapo yaweze kutibiwa mapema.

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wanawake milioni 7.1 wanagundulika na saratani hiyo kila mwaka duniani, hivyo kuufanya ugonjwa huo kuwa tishio kwa wanawake wakati hapa nchini uelewa mdogo unatajwa kuwa ni moja ya sababu za ongezeko lake.

Dk. Christopher Peterson anasema ili kuepusha saratani ya matiti ni vema jamii ikajenga utaratibu wa kupima saratani mara kwa mara kwani ikigunduliwa katika hatua za awali inatibika.

Wanawake wengi wanapoteza maisha kwa sababu ya kuchelewa kupata vipimo ambavyo wangepatiwa mapema ingesaidia kutibiwa kwa wakati.

Dokta Peterson anataja dalili za ugonjwa huo kuwa ni maumivu chini ya kwapa na kwenye matiti yanayotokea mara kwa mara, rangi ya ngozi ya titi kubadilika kuwa nyekundu au kama chungwa, muonekano wa chuchu nao kubadilika ambapo hutoa kimiminika chenye mchanganyiko wa damu.

“Pia kunakuwa na mabadiliko ya kimaumbile na ukubwa wa titi na dalili nyingine kuu ni kuhisi uvimbe mgumu unaoanza kujitokeza kwenye titi moja na mara nyingi hautoi maumivu.

“Angalizo ni kwamba si kila uvimbe kwenye titi unaashirika saratani ni vema kujenga utamaduni wa kupima mara kwa mara hasa unapohisi una uvimbe kwenye titi,”anasema.

Hapa nchini tatizo la saratani limekuwa likiongezeka kila mwaka huku WHO ikikadiria kuwa kila mwaka wagonjwa wapya 50,000 wanagundulika na saratani za aina mbalimbali hapa nchini, huku 13,000 miongoni mwao ambao ni sawa na asilimia 26 ndiyo wanafanikiwa kufika hospitali kupatiwa matibabu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema mwaka 2017 serikali iliongeza vituo 100 kutoka 343 vilivyokuwa awali kwa ajioli huduma za kupima matibabu ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na ugonjwa huo.

"Zahanati, vituo vya afya na hospitali tumevipatia vifa tiba na utaalamu ili kuwezesha wanawake wengi kupima saratani ya kizazi na matiti pamoja na kupata matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya kizazi papo hapo.

“Tumelenga kuwafikia wanawake milioni 3 nchini ifikapo Desemba 2018,” anasema Waziri Ummy.

Aidha, waziri huyo anasema pia serikali inaendelea na jitihada za kusogeza huduma za matibabu ya saratani kwa njia ya mionzi katika hospitali za Rufaa za Kanda (Mbeya, Bugando na KCMC).

“Pia tunaendelea nkuimarisha huduma za matibabu ya saratani katika Hospitali ya Ocean Road kwa kuweka mashine mbili mpya za kisasa ambazo zitasaidia kupunguza muda wa kusubiri kwa wagonjwa kupata huduma za tiba ya mionzi sanjari na kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100,”anasema waziri huyo anayehusika masuala ya afya nchini.

No comments:

Post a Comment