Tuesday, 10 April 2018

Serikali: Hakuna dhamana nyingine ya mtumishi kukopea zaidi ya mshahara wake


Joseph Kakunda 

NAIBU waziri OR-Tamisemi, Joseph Kakunda amesema hakuna dhamana ya mtumishi kukopa katika benki au taasisi zaidi ya dhamana ya mshahara wake kinachotakiwa asiwe anadaiwa mikopo mingine.

Kakunda ameyasema hayo leo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge Grace Tendega aliyehoji  kwanini walimu wamekuwa wakikosa mikopo kwa kukosa udhamini katika benki mbalimbali.

Katika swali lake Tendega alihoji; Je serikali haioni haja kuwa ni wakati muafaka mifuko ya hifadhi ya jamii iweze kufanya dhamana kwa walimu wetu wakati wakiwa kazini na sio baada ya kustaafu?

"Karibu mabenki yote na taasisi zote hakuna dhamana zaidi ya mshahara wa mtumishi, kinachotakiwa asiwe anadaiwa mikopo mingine hilo ndio jambo la msingi na kama hadaiwi mikopo mingine anao uwezo wa kukopa na ataamua mwenyewe akope kwa kurejesha miaka mitatu au 10 au hata miaka 25.

"Ni yeye mwenyewe katika makubaliano ya sehemu yake kwa hiyo napenda kuwasisitiza watumishi wote nchi nzima na wakurugenzi wa halmashauri ambao wako chini yangu kwamba mikopo hiyo ya watumishi ipo, waingie katika makubaliano maalum na hizo taasisi na mabenki ili watumishi waweze kukopeshwa na wajenge nyumba zao binafsi,” amesema naibu waziri Tamisemi, Joseph Kakunda.

No comments:

Post a Comment