Tuesday, 17 April 2018

Serikali imedhibiti uvuvi haramu - Makamba


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba (wa pili kulia) akizungumza baada ya mchakato wa upandaji miti ya mikoko eneo la baharini mkoani Tanga.

Mwandishi Wetu, Tanga

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
January Makamba amesema serikali imefanikiwa kudhibiti matukio ya uvuvi haramu kwa zaidi ya asilimia 80 katika maeneo ya bahari na maziwa baada ya kuimarisha doria na ukaguzi wa samaki wanaovuliwa.

Ameyasema hayo wakati wa upandaji wa mikoko katika Pwani ya Bahari ya Hindi ambayo ilipandwa eneo la Mwambani jijini Tanga chini ya udhamini wa mfuko wa Vodacom.

Amesema kuimarika kwa doria hizo kumesaidia wananachi kuwa na uelewa mpana kuhusu madhara ya uvuvi haramu na hivyo kuanza kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo ikiwemo ulinzi wa mazingira ya Bahari ya Hindi na rasilimali zake.

Waziri huyo amesema pamoja na jitihada za wizara katika kudhibiti fukwe za bahari zisiendelee kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi lakini bado kuna maeneo mengi ambayo yanahitaji kuhifadhiwa kwa kupandwa miti ya mikoko.

Pamoja na hayo waziri huyo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru
Vodacom Foundation kwa kuja na kampeni ya upandaji mikoko ili kuhifadhi mazingira ya bahari kwa kile alichosema kutasaidia kuboresha mazingira hayo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Vodacom Foundation, Rosalynn Mworia amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na chama cha skauti Tanzania waliamua kuja na kampeni hiyo ya upandaji wa mikoko ili kuhifadhi mazingira ya fukwe.

Amesema kwa kuanza kampeni hiyo wameanzia na mkoa wa Tanga na wanatarajia kuipeleka nchi nzima ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.(Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)

No comments:

Post a Comment