Thursday, 12 April 2018

Serikali imejitahidi kupunguza hati chafu – CAGMdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Assad (katikati) akizungumzia kuhusu serikali kuweka vizuri hesabu zake na hivyo kupungua hati chafu.

Mwandishi Wetu, Dodoma

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli inaendelea vizuri na uwekaji wa hesabu uliopelekea kupungua kwa hati chafu katika taasisi na miradi mbalimbali ya Serikali.

Prof. Assad ameyasema hayo jana mjini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2017.

“Katika ukaguzi wa hesabu nilioufanya katika Serikali Kuu na taasisi zake, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2016/17 nimetoa hati 561 za ukaguzi.

“Kati ya hati hizo, zinazoridhisha ni 502 sawa na asilimia 90, hati zenye shaka ni 45 sawa na asilimia 90, zisizoridhisha ni Saba sawa na asilimia Moja na mbaya ni Saba sawa na asilimia Moja,” amesema Prof. Assad.

Ameongeza kuwa katika ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na taasisi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ametoa hati za ukaguzi 742 ambapo zinazoridhisha ni 697 sawa na asilimia 94, hati zenye shaka ni 44 sawa na asilimia 5.9 na isiyoridhisha ni moja, ambayo  imetolewa kwa mradi wa maji (WSDP) unaotekelezwa na mamlaka za Serikali za mitaa ya wilaya ya Makete.

Naye, mjumbe wa kamati ya LAAC,  Abdallah Mtolea amezipongeza halmashauri zilizofanya vizuri kwa kuonekana kupunguza idadi ya hati chafu na kushamiri kwa hati safi.

Aidha Mtolea amesema kamati yake itaziita halmaushari na kufanya nazo mahojiano bila kujali matokeo ya ukaguzi kama zilifanya vizuri au vibaya ili kuhakikisha kuna kuwa na matumizi mazuri ya fedha za umma.

No comments:

Post a Comment