Thursday, 5 April 2018

Serikali kuendeleza mkakati wa huduma bora za afya kwa wananchi


Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo, Constantine Mushi alipozindua mafunzo kwa wakufunzi (hawapo pichani), jijini Mbeya jana.

Mwandishi Wetu, Mbeya

SERIKALI imesema inaendelea na mkakati wa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za afya na kwa wakati ili kuleta ustawi katika kufikia azma ya Tanzania ya viwanda.

Hayo yamebainishwa jana jijini Mbeya na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo, Constantine Mushi alipokuwa akizinduzi mafunzo kwa wakufunzi wa kitaifa kuhusu Bima ya Afya ya Jamii (CHF), mfumo wa kupeleka fedha moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma (DHFF), na mfumo wa ununuzi wa dawa nje ya mfumo wa kawaida wa MSD (Jazia – Prime Vendor System).

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini Rais Dk. John Magufuli imedhamiria kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya ya uhakika kwa kupata huduma bora za afya na kwa wakati, jambo lililopelekea kuanzishwa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

“Lengo mahsusi ya mafunzo haya ni kuelewa kwa upana maana ya ugatuaji wa mipango ya afya na bajeti kwa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma (DHFF)”yenye matarajio ya kupunguza urasimu na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa  kuimarisha uwajibikaji na uboreshaji wa uandaaji wa mipango, bajeti na matumizi  yanayolenga kuboresha huduma za afya,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa hadi sasa robo ya pili ya mwaka Serikali imesha peleka sh. bilioni 45 katika vituo vya kutolea huduma za afya 5,125 nchi nzima.

Aidha Mushi ambainisha kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa afya kwa wananchi wake imekuwa na mikakati ambayo inashirikiana na wadau wa maendeleo katika kuitekeleza ikiwemo utekelezaji wa maboresho ya mifumo ya sekta za umma inayoratibiwa na Tamisemi kwa ufadhili wa Serikali ya Watu wa Marekani kupitia Shirika lake la maendeleo USAID/PS3 ambao unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania Bara.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo ambao tumeendelea kushirikiana nao katika nyanja mbalimbali, kwa kipekee niwashukuru wenzetu Wadau wa Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund), HPSS, PS3, Global Supply Chain Program, Boresha Afya – Deloitte, World Vision. EGPAF, Jhpiego, GIZ, AGPAHI na Pharmaccess,” ameongeza.

Akitoa muongozo wa mafunzo hayo mwakilishi kutoka OR- Tamisemi Nkinda Shekalage amesema mafunzo haya yataleta chachu katika kufikia malengo ya utoaji wa huduma za afya zilizo bora na kwa ufanisi endapo washiriki wataenda kutekeleza wajibu wao wa kuwafundishi walio chini yao kama ilivyokusudiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Fedha wa PS3, Dk. Gemini Mtei amesema PS3 imeshirikiana na Ofisi ya Rais – Taisemi kuiunda DHFF kwa ajili ya kuwezesha vituo vya kutolea huduma za afya kupokea fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja(HBF) moja kwa moja kwenye akaunti zao. 

Dk. Gemini amesema msaada uliotolewa na PS3 ni wa kitaalam, ili kuwezesha kuwepo mfumo mzuri wa upokeaji wa fedha hizo sanjari na hilo, PS3 imeshirikiana na Serikali kuweka mifumo itakayowezesha DHFF kufanikiwa, mifumo hii ni Mfumo wa Uhasibu na Utoaji Taarifa kwenye Vituo vya Kutolea Huduma (FFARS) pamoja na mfumo wa mipango, bajeti na utoaji wa taarifa (PlanRep). 

Ameongeza PS3 itaendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza uimarishwaji mifumo mbalimbali inayolenga kuboresha sekta ya afya na sekta nyingine kulingana na mahitaji ya Serikali.

Mradi wa PS3 umesaidia pia kujenga uwezo kwa Serikali katika maeneo ya utekelezwaji wa mpango wa DHFF, CHF iliyoboreshwa, na PV.  USAID kupitia PS3 imewezesha mafunzo ya wakufunzi wa kitaifa yaliyofanyika mjini Morogoro wiki moja iliyopita, na pia ndiyo inayofadhili mafunzo yaliyoanza jana kwenye mikoa mine ya Mbeya, Mwanza, Morogoro na Mtwara. 

Mafunzo haya yamehusisha maofisa kutoka mikoa yote ya Tanzania bara, na baadaye yatashuka kwenda ngazi ya halmashauri na kwingineko.

No comments:

Post a Comment