Saturday, 7 April 2018

Serikali yafafanua takwimu za vifo vya uzazi nchini


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile.

Peter Simon

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa ufafanuzi wa takwimu za vifo vinavyotokana na uzazi nchini.

Ufafanuzi huu umekuja baada ya taarifa iliyorushwa na kituo cha Televisioni cha ITV katika moja ya taarifa zake za habari Machi 29, 2018 na baadaye kuanza kuzunguka katika mitandao ya kijamii inayosema;

“Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu-UNFPA limesema idadi ya vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na uzazi hapa nchini vimeongezeka hadi kufikia vifo 556 kwa kila vizazi hai 1000 kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya ikiwamo uhaba wa wauguzi na wakunga.

“Nikiwa waziri mwenye dhamana ya afya, napenda kuufahamisha umma kuwa taarifa hizo sio sahihi. 

“Na ukweli wake ni kuwa takwimu za tathmini iliyofanywa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2015/2016 (Ikiwa ni miaka miwili na nusu iliyopita), Hali ya Afya za Watu Tanzania (TDHS – MIS) ni kuwa vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi ni 556 kwa kila vizazi hai 100,000 na si vifo 556 kwa kila vizazi hai 1,000.  Aidha nasisitiza kuwa takwimu hizi ni za miaka miwili na nusu iliyopita.

“Ni muhimu ikafahamika kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tangu imeingia madarakani Novemba 2015, imewekeza sana katika sekta ya afya hususan katika eneo la afya ya mama na mtoto. 

Tuna imani kuwa endapo itafanywa tathmini kama hii iliyofanywa na kusimamiwa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hakuna shaka kuwa itatuonesha hatua kubwa tuliyopiga katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo tumechukuwa hatua mbalimbali zenye lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Mikakati ambayo serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya Afya imewekeza na kuitekeleza  ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ni pamoja na:-

Kuandaa na kuanza utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka 5 wa mwaka 2016 hadi 2020 unaolenga kuboresha afya ya uzazi, watoto na vijana pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 292 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020.

Mpango huu umezingatia maeneo makuu matatu: ambayo ni: huduma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua. Utekelezaji wa mpango huu unaelekeza sekta ya afya katika kujikita kwenye afua muhimu za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Kuongeza uwajibikaji kwa ngazi zote ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kutaka kila kifo cha mama na mtoto kinachotokana na matatizo ya uzazi kitolewe taarifa ndani ya saa 24 katika kituo cha huduma au ngazi ya jamii kilipotokea na baadaye kujadiliwa ili kubaini chimbuko la kifo hicho na kuchukua hatua stahiki hasa kwa kutatua changamoto zinazojitokeza. 

Hatua hii imeanza kutekelezwa tangu Oktoba 2016 na imekuwa chachu katika kuboresha huduma kwa kina mama wajawazito nchini.

Wizara kwa kushirikiana na OR – Tamisemi na wadau mbalimbali, inaendelea na kazi ya kukarabati vituo vya afya, zaidi ya 220 katika halmashauri mbalimbali nchini kwa kujenga na kukarabati majengo ya upasuaji,  wodi za wazazi na watoto, maabara ya damu na nyumba za watumishi ili kusogeza karibu na wananchi huduma za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.

Hadi Desemba 2015, ni vituo vya afya vya serikali 117 tu sawa na asilimia 21 kati ya vituo vya afya vya 473 vinavyoweza kutoa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito. 

Hakuna shaka kuwa jitihada hizi za Serikali ya Awamu ya Tano za kupanua huduma za upasuaji wa dharura zitaokoa maisha ya kinamama wajawazito na vichanga vyao.

Huduma za rufaa kwa wajawazito zimeendelea kuboreshwa ambapo Serikali imegawa magari ya kubebea wagonjwa zaidi ya 100 katika kuimarisha juhudi za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi katika mikoa ambayo takwimu zimeonesha kuwa ina vifo vingi zaidi vitokanavyo na uzazi.

No comments:

Post a Comment