Friday, 6 April 2018

Serikali yaungana na China kumbukumbu vifo vya wajenzi reli ya TazaraWaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Kikanda na Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustino Mahiga akizungumza wakati wa kumbukizi hizo.

Peter Simon

SERIKALI imeungana na Jamhuri ya Watu wa China katika kumbukumbu ya vifo vya Wachina 70 waliofarika wakati wa ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).

Watanzania waliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Kikanda na Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustino Mahiga huku ikiwakilishwa na Balozi wao nchini, Wang Ke.

Kumbukumbu hiyo, imeandaliwa na Jumuia ya Marafiki wa Tanzania na China ambayo Mwenyekiti wake Dk.Salim Ahmed Salim na Katibu wake ni Joseph Kahama.

Kabla ya kuweka mashada kwenye makaburi ya Wachina hao ambao wengi wao ni wataalamu na wahandisi katika ujenzi wa reli, ilitolewa historia fupi ya vifo vyao.

Akizungumza baada ya kuweka mashada, Balozi Dk. Mahiga amesema ujenzi wa reli hiyo ulithibitisha urafiki wa kutoka moyoni kati ya nchi hizo mbili na kufafanua ujenzi wake ulifungua milango kwa China kujenga viwanda vingine kama Ufi na kiwanda cha nguo cha Urafiki.

“Wakati wa ujenzi huu damu zilimwagika, Wachina wamepoteza maisha na wengine wamebaki na ulemavu wa kudumu…hivyo urafiki wetu sisi na China ni wa damu,” amesema.

Naye, Balozi Wang amesema nusu ya karne iliyopita, kupitia ombi la Rais wa Tanzania, Julius Nyerere na Rais wa Zambia, Kenneth Kaunda, viongozi wa kizazi cha China, Mwenyekiti Mao Zedong na Waziri Mkuu, Zhou Enlai walifanya uamuzi wa kimkakati na kihistoria kusaidia ujenzi wa Tazara.“Wafanyakazi na mafundi Wachina 50,000 waliitikia wito wa taifa na waliungwa mkono na wenzao kutoka Tanzania na Zambia, walishinda vigumu na vikwazo vingine kumalizia ujenzi wa Tazara yenye urefu wa kilomita 1,860 ndani ya miaka sita na kuufanya kuwa  mradi wa kihistoria wenye umaarufu duniani,”amesema.

Amesema wafanyakazi na mafundi 65  Wakichina walipoteza maisha na walizikwa katika ardhi ya Afrika mbali na nyumbani kwao.

Tazara imekuwa ikifahamika kwa dunia kama reli ya ukombozi iliyowasaidia watu wa Afrika kupata Uhuru na Ukombozi…na pia reli ya urafiki ikiwakilisha urafiki wa ndani kati ya Wachina na Waafrika,”amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema ipo haja kwa Tanzania na China kuendelea kudumisha urafiki wao.

“Wakati ule Mwalimu Nyerere kabla ya kwenda kuomba China watujengee reli alianza kuomba kwa nchi moja ya Magharibi siitaji, anayetaka kuijua aje nitamnong’oneza. Nchi hiyo ilimjibu Nyerere hivi; ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia upitie Zanzibar. Nyerere akaondoka tukaenda China na baada ya kufika huko Mwalimu ikabidi aongee na waziri mkuu wa nchi hiyo, Zhou Enlai.

“Tena wakati anaomba hakwenda moja kwa moja alizunguka lakini hakujibiwa chochote ila wakati tunataka kuondoka tulienda kuaga kwa Rais wa China ambaye alikubali ombi letu. Kwa hiyo huu ni urafiki wa damu,” amesema Butiku.

No comments:

Post a Comment