Sunday, 22 April 2018

Sido yawakumbuka wenye uthubutu


Mkurugenzi wa kampuni za Mandai, ambaye pia ni mtaalam wa tiba, lishe na virutubisho, Abdallah Mandai (kushoto), akitunukiwa cheti na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (Sido) mkoa wa Dar es Salaam, Mackdonald Maganga wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti maalum wajasiriamali waliothubutu kuanzisha viwanda vidogo iliyofanyika Ijumaa Aprili 20, 2018, Dar es Salaam.


Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki wa hafla ya kutunukiwa vyeti maalum kwa wajasiriamali waliothubutu kuanzisha viwanda vidogo jijini Dar es Salaam, iliyoandalliwa na Sido na kufanyika Ijumaa Aprili 20, 2018. 
Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), mkoa wa Dar es Salaam, limewatunuku vyeti maalumu wajasiriamali wapatao 300 wa mkoa huo waliothubutu kuanzisha viwanda vidogo.

Akizungumza katika hafla ya kutunuku vyeti kwa wajasiriamali hao, iliyofanyika Dar es Salaam juzi Ijumaa, mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva amewataka wajasiriamali hao kuwa wazalendo katika kulipa kodi.

Wakati huo huo, kaimu Mkurugenzi wa Sido, Joyce Temu amewataka wajasiriamali kurasimisha biashara zao ili waweze kutambulika katika utolewaji wa fursa.

Naye Mkurugenzi wa kampuni za Mandai, Abdallah Mandai ambaye ni mmoja wa watunukiwa wa vyeti hivyo, amesema kilichofanywa na Sido ni kielelezo kuwa serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuifikisha nchi kwenye uchumi wa viwanda kama ilivyo kusudio lake.

Amesema katika awamu zilizopita taasisi mbalimbali za serikali kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), zilikuwa ni sehemu nyeti kuingilika tofauti na ilivyo sasa.

Amesema sasa zipo karibu na wananchi na pia hata tozo zao katika kuangalia jengo linalotakiwa kuanzishwa kiwanda zimeshuka hali ambayo inatoa fursa kwa wengi kuthubutu kuanzisha viwanda vidogo na hata vya kati.

Kuhusu Sido amesema utaratibu wao kuwapa vyeti wathubutu ni mzuri kwani unatoa hamasa kwa wanaotaka kuanzisha viwanda au biashara kutimiza kusudio lao.

Pia amesifu utaratibu walio nao Sido kwa sasa wa kuwafundisha watu namna kuanzisha viwanda vidogo na kisha kusimamia kazi walizowafundisha ambazo wanaendelea kuzifanya wao.

Kwa upande wake Rais wa Sauti ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania- Vowet, Maida Waziri ambaye ni miongoni mwa wajasiriamali waliotunukiwa vyeti hivyo kutokana na kuanzisha kiwanda cha utengenezaji thamani-Ibra Enterprises LTD, ameishukuru Sido kwa kuutambua mchango wake. 

“Nimefarijika kwa kazi iliyofanywa na serikali kupitia Sido imetambua na kuthamini mchango wa wajasiriamali itatupeleka mbele zaidi imetuhamasisha na kutuvuta zaidi, mwito wangu kwa wajasiriamali wote hasa wanawake wajitokeze kurasimisha viwanda vyao watatambulika na kupata fursa zilizoko jirani yetu,” amesema.

No comments:

Post a Comment