Wednesday, 11 April 2018

Talgwu ‘yampa tano’ Musukuma


Musukuma akichangia hoja bungeni mjini Dodoma.


CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu), kimefunguka na kumwagia sifa Mbunge wa jimbo la Geita Mjini, Joseph Kasheku maarufu kama Musukuma kwa kulivalia njuga suala la watumishi wa umma waliofukuzwa kazi wenye sifa ya darasa la saba, na hadi serikali kuamua kuwarudisha kazini.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashid Mohamed Mtima  wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari jana ikiwa ni siku moja tangu serikali ilivyotoa kauli ya kurudisha kazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika ndiye aliagiza watumishi wa umma 1,370 walioajiriwa kabla ya Mei 20, 2004 ambao hawakufaulu mtihani wa kidato cha nne na waliondolewa kazini kwa kigezo cha vyeti vya kidato cha nne, warudishwe kazini mara moja na wapewe stahiki zao ikiwemo mishahara yate ya tangu walipoachishwa kazi.

"Suala hili sisi tumeanza muda mrefu kulihangaikia lakini ‘last week' tuliwaona wabunge walivyokuwa wamechachamaa Bungeni wakiongozwa na Mbunge wa Geita Mjini, Musukuma kwa kuweza kulipigia kelele jambo hili.... tunawashukuru sana, kwa maana hata kama lingekuwa lipo kwenye mchakato la kufanyiwa kazi lakini wao waliliongezea kazi zaidi hadi serikali ikatangaza kuwarudisha kazini," amesema Mtima.

Pamoja na hayo, Mtima ameendelea kwa kusema "kwa niaba ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu), napenda kutoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuzingatia mapendekezo tuliyowasilisha serikalini Machi 22, 2018 na hatimaye jana (juzi) yakafanyiwa kazi. 

"Kwa kweli jambo hili tunashukuru sana kwa maana serikali imekuwa sikivu. Pia tunapenda kutoa shukrani kwa Waziri Mkuu kwa namna alivyoweza kutusaidia kipindi tulivyokuwa tunahangaikia mchakato huu".

Kwa upande mwingine, Mtima amesema wanachama wake wamefurahishwa na uamuzi huo wa serikali kwa kuwa umeweza kurudisha matumaini mapya kwa watumishi hao waliofukuzwa kazi hapo awali.

No comments:

Post a Comment