RAIS wa Marekani, Donald Trump ameahidi " kutumia nguvu "
kujibu madai ya shambulio la kemikali nchini Syria, huku mataifa ya magharibi
yakitafakari hatua yatakayoichukulia.
"Tuna njia
nyingi za kijeshi,"aliwambia waandishi wa habari. Ameongeza hatua ya
kujibu shambulio hilo itaamuliwa katika kipindi cha "muda mfupi".
Trump amesema Marekani
inapata ''msaada mzuri" kuhusu nani aliyehusika na shambulio la Douma
Jumamosi.
Duru za
kitabibu zinasema makumi kadhaa ya watu waliuawa katika shambulio hilo, lakini
idadi kamili haijathibitishwa.
Trump pia amejadili
tukio hilo la rais wa Ufaransa Emmanuel Macron jana Jumatatu jioni na viongozi
wote walielezea utashi wao wa "kujibu kikamilifu".
Waziri Mkuu wa
Uingereza, Theresa May amesema "analaani vikali" kitendo cha
"ukatili" kinachodaiwa kuwa ni shambulio la kemikali na akatoa mwito
kwa wanaomuunga mkono rais Bashar al-Assad kuwajibishwa.
Kauli za
viongozi wa kimagharibi za kulaani shambulio hilo zimefuatia kikao cha
malumbano katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Marekani na Urusi
walitupiana maneno makali kuhusiana na tukio la Douma.
Mwakilishi wa
Urusi kwenye baraza hilo, Vassily Nebenzia amesema shambulio hilo linadaiwa
lilipangwa na akaonya kwamba hatua za kijeshi za Marekani zinazolenga kujibu
tukio hilo "zitakuwa na athari mbaya".
Mjumbe wa
Marekani Nikki Haley amesema wanaounga mkono jeshi la Syrian - wana "damu
ya watoto wa Syria " mikononi mwao na akambandika jina rais Assad kama
"zimwi ".
Haley ametoa mwito
wa kupigwa kura kuhusu muswada wa maazimio ya kubuniwa tume ya uchunguzi ya
matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria siku ya Jumanne.
Lakini Urusi
inasema haiwezi kuunga mkono pendekezo hilo kwasababu lina "vipengele
visivyokubalika''.
Shirika la
matibabu la Marekani na Syria linasema watu zaidi ya 500 waliletwa kwenye kituo
cha matibabu katika mji wa Douma, uliopo jimbo la mashariki la Ghouta, karibu
na mji mkuu Damascus, wakiwa na dalili "zinazoonesha kuwa walishambuliwa
na kemikali".
Shirika hilo
linasema dalili walizokuwa nazo ni pamoja na ugumu wa kupumua, ngozi ya
samawati , kutokwa na povu mdomoni , kuungua kwa mboni na "walikuwa na
harufu kama ya kemikali ya chlorine".
Idadi kamili ya
vifo ya na ni nini hasa kilichotokea haviwezi kuthibitishwa kwasababu eneo hilo
halina mawasiliano.
Makadirio ya
idadi ya watu waliouawa katika shambulio hilo linaloshukiwa kuwa la kemikali ni
kuanzia watu 42 hadi zaidi 60, lakini makundi ya kitabibu yanasema idadi hiyo
inaweza kuongezeka baada ya wahudumu wa uokoaji kuweza kufika kwenye sehemu za
chini za majengo ambako mamia ya familia walikuwa wamekimbilia kuepuka
mashambulio ya mabomu.
Mwakilishi wa
Ufaransa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema gesi ya sumu
ilitumiwa kwa makusudi kwasababu inaweza kusambaa hadi sehemu za chini za
majengo.
Marekani, Ufaransa
na Uingereza wameongoza kampeni ya kimataifa ya kulaani shambulio hilo
linalodaiwa kuwa la kemikali, huku serikali ya Syria na waungaji mkono wao
Urusi wakikana kuwajibika kwao kokote na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment