Tuesday, 3 April 2018

Tumbili aiba mtoto, atoroka naye


Top of Form

POLISI nchini India wanamsaka tumbili mmoja ambaye aliiba mtoto na kutoroka naye katika jimbo la Orissa, mashariki mwa nchi hiyo.
Mwili wa mtoto huyo ulipatikana baadaye kwenye kisima. Mama wa mtoto huyo wa kiume anasema alishuhudia kisa hicho kikitokea lakini hakuweza kumuokoa.
Jamaa wake aliupata mwili wa mwanawe huyo kwenye kisima nyuma ya nyumba yao, siku moja baada ya motto huyo kuibwa na tumbili huyo.
Mnyama huyo alikuwa ameingia ndani ya nyumba ya familia hiyo na kumtwaa mtoto huyo.
Polisi wanasema kisa hicho ni cha kipekee sana, ingawa mara kwa mara tumbili hupatikana wakiharibu mali eneo hilo.
"Tunatumai kwamba tutafanikiwa kumkamata tumbili huyu katika kipindi cha wiki moja," ofisa mmoja wa polisi kwa jina Pradhan ameambia BBC.
"Ingawa visa vya tumbili kuwashambulia binadamu au kuingia kwenye nyumba za watu wakitafuta chakula ni vya kawaida, hiki ndicho kisa cha kwanza kwa tumbili kutoroka na mtoto," ameongeza.
Polisi wanashirikiana na watu wa eneo hilo, ambao ni stadi wa kuwakamata tumbili.
Maofisa wa idara ya msitu wameiambia BBC kwamba tumbili huyo aliingia kwenye nyumba ya familia hiyo Jumamosi asubuhi na kutoroka na mtoto huyo.
Daktari aliyeuchunguza mwili wa motto huyo anasema haukuwa na alama za majeraha.
"Inaonekana alifariki kutokana na kukosa hewa pengine kutokana na kuzama kwenye maji kisimani," amesema daktari huyo.
Wakazi wamewaambia wanahabari kwamba huenda tumbili huyo alimwangusha mtoto huyo akitoroka.

No comments:

Post a Comment