Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala (kulia), akizungumza na balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke afisini kwake mjini Dodoma.
Mary Meshack, Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla
amesema serikali imefanikiwa kudhibiti vitendo ya ujangili hapa nchini kwa
zaidi ya asilimia 50.
Amesema hayo jana wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa
nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma.
Mazungumzo hayo yalilenga kujadili mambo mbalimbali ikiwemo
kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta ya uhifadhi na
maendeleo ya utalii.
Dk. Kigwangalla amesema katika kipindi cha miezi sita
iliyopita hakuna mauaji mapya ya wanyamapori yaliyoripotiwa na kwamba nyara
zinazokamatwa hivi sasa ikiwemo meno ya tembo na ngozi za wanyamapori ni
masalia ya zamani.
Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi mbalimbali
zinazofanywa na Serikali kudhibiti vitendo vya ujangili ikiwemo doria za mara
kwa mara za kiitelijensia ambazo zimekuwa zikishirikisha vyombo mbalimbali vya
ulinzi na usalama pamoja na raia wema.
Kwa upande wake balozi Cooke amesema nchi yake itaendelea
kuimarisha ushirikiano inaoutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kudhibiti
mtandao wa uhalifu wa dawa za kulevya, rushwa na ujangili.
Amesema kwa sasa watalii zaidi ya 75,000 wa Uingereza
hutembelea Tanzania kila mwaka na wengine wamewekeza katika sekta ya utalii
hapa nchini, hivyo ameiomba Serikali kurekebisha baadhi ya changamoto zilizopo
katika sekta hiyo kwenye mtiririko wa kodi.
No comments:
Post a Comment