Friday, 13 April 2018

Ujerumani haitashiriki vita Syria


Angela Merkel 
KANSELA wa  Ujerumani Angela Merkel amesema shambulio la gesi ya sumu linalodaiwa kufanywa na serikali ya Syria linadhihirisha utawala wa Rais Bashar al-Assad umeshindwa kutokomeza hazina yake ya silaha za sumu.

Rais  wa  Marekani Donald Trump amesema shambulio  dhidi  ya  Syria  huenda  likafanyika "hivi  karibuni  ama hata  sio  hivi  karibuni  kabisa"  akidai  kwamba  hajawahi kuashiria muda  wa  kujibu  shambulio  hilo la  gesi  ya  sumu , suala aliloonesha  ishara kwamba lingefanyika hivi  karibuni. 

Kansela  Merkel  amesema ," Tunapaswa  kukiri  kwamba  ni dhahiri  hatua  za  kuharibu  silaha  hizo  za  sumu  hazikufanyika kwa ukamilifu," amesema , sio  kwamba  hakuna  ushahidi  wa  kutosha kwamba  serikali  ya  Syria  ilitumia  silaha  hizo  za  sumu. 

Serikali ya  Syria  iliepuka  mashambulizi ya Marekani na Ufaransa mwaka 2013 katika kujibu shambulio linaloshukiwa kuwa ni la gesi ya sarin kwa  kukubali kukabidhi hazina yake ya silaha za sumu.

Kutokana na madai ya matumizi ya gesi ya sumu katika eneo lililokuwa  linashikiliwa na waasi la Douma, Rais Trump  wiki  hii aliongeza mbinyo  dhidi ya Damascus, akionya katika maandishi yake kadhaa katika mtandao  wa kijamii wa Twitter kwamba

"makombora yanakuja" ili  kulipiza  kisasi. Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov hata hivyo amesema Urusi inafuatilia kwa karibu taarifa  zinazotoka Marekani.

"Urusi  inafuatilia  kwa  karibu  matamshi  kutoka Marekani na bado tunaamini kwamba  ni muhimu sana kuepuka hatua zozote ambazo zitaweza kusababisha msuguano nchini Syria. Tunafikiri  hali  hiyo italeta  athari mbaya katika mchakato mzima wa utulivu wa Syria."

Ujerumani haitashiriki vita

Kansela Merkel  amesema "hatua  kadhaa " zitatiliwa maanani kujibu  shambulio hilo la gesi ya sumu, lakini aliondoa uwezekano wa hatua za  kijeshi. Ujerumani haitashiriki kijeshi, lakini itatoa msaada iwapo wawakilishi katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wataamua  kuchukua hatua mbali na hatua za kidiplomasia" amesisitiza.

Ufaransa lakini inatarajiwa kujiunga na Marekani na Uingereza kufanya  mashambulio ya anga ama njia nyingine za mashambulio kujibu shambulio  hilo la silaha za sumu, lakini inabaki bila uhakika iwapo hilo huenda  likatokea ama hata iwapo kweli litatokea.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema leo kwamba nchi yake inaushahidi kwamba serikali ya Syria ilifanya shambulio hilo la silaha za  sumu wiki iliyopita na itaamua iwapo ishambulie wakati taarifa zote  muhimu zitakapokuwa zimekusanywa.

"Kuna mfumo  wa  sheria  za  kimataifa, tuna ushahidi  kwamba  wiki iliyopita shambulio la gesi ya sumu ya klorine lilifanyika na kwamba   lilifanywa na serikali ya Bashar al-Assad.

Sheria za kiutu  na kutoa nafasi  kwa  misaada  ya  kiutu, kusaidia  asasi zisizo za  kiserikali  kuwasaidia  watu ndani  ya  nchi  hiyo, katika njia  kwenda Idlib na kuwatoa  raia  kutoka  katika  eneo  hilo.

Watoto  pamoja  na  wanawake.  Ili  kutoona  tena  picha  za  kutisha za  uhalifu  ambapo  tuliona  watoto  na  wanawake  wakifariki kutokana  na  kushindwa kupumua."

Rais  wa  Marekani  Donald Trump ameandika  katika  ukurasa  wa Twitter leo  asubuhi, "Sijasema  lini shamabulio dhidi  ya  Syria litafanyika. Huenda  ni  hivi  karubuni ama  hata  pengine sio  hivi karibuni kabisa !
“Wakati  huo  huo meli  za  kijeshi  za Urusi zimeondoka  kutoka katika  vituo vyake  katika  bahari  ya Mediterania  kwa kile kilichoelezwa kuwa ni  usalama wake, hali iliyoelezwa na makamu mwenyekiti wa kamati ya  ulinzi ya Urusi kwamba ni hatua za kawaida, wakati kuna kitisho cha shambulio.

Chanzo:DW

No comments:

Post a Comment