Monday, 23 April 2018

Ukimwi,kifua kikuu sasa kupimwa baa


Dk. Faustine Ndugulile 

Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imesema katika mikakati yake ya kuwatambua wagonjwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi na TB imeazimia kutembelea maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi ikiwemo baa na migodini ili kuwafikia watu kwa urahisi hususan wanaume.

Hayo yameelezwa leo Aprili 23, 2018 Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara Afya, Dk. Faustine Ndugulile wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah aliyetaka kufahamu serikali ina mikakati gani katika kutoa elimu maalum ambayo itaweza kuenea kwa kasi zaidi katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi zaidi.

Dk. Ndugulile amesema mara baada ya serikali kuona kumekuwa na changamoto kubwa sana katika utambuzi wa makundi maalum ambayo wengi wamekuwa wakiathirika na ugonjwa wa TB na Ukimwi, waliamua kujielekeza kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari.

“Lakini vilevile tuna mkakati mahsusi wa kuwatafuta wagonjwa wa TB katika migodi sanjari na hilo tumeweka mikakati jumuishi kati ya ugonjwa wa TB na Ukimwi.

“Sasa hivi tumeanza kujielekeza mahali kwenye watu wengi ili tuweze kuwapata kwa pamoja hususan wanaume ambapo mara nyingi wanakuwa katika baa. Msishangae kutuona na sisi tunapita huko kuwaomba kufanya upimaji wa ugonjwa wa Ukimwi pamoja na TB,” ameongeza.

Katika hatua nyingine Dk. Ndugulile amesema kumgundua mgonjwa wa TB mapema na kumweka katika matibabu ndio njia kuu ya kupambana na kulishinda tatizo la kifua kikuu jambo ambalo lipo kwenye mikakati ya serikali.

No comments:

Post a Comment