Sunday, 8 April 2018

Wadau wa usafiri Tabora wataka malori nayo yatumie 'Log book' kudhibiti ajali

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey  Mwanri (katikati) akifafanua jambo jana wakati wa kikao cha kutathmini ili kuja na majibu ya kuondoa ajali za barabarani mkoani humo kichofanyika wilayani Igunga na kuhudhuriwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Tabora na ile ya wilaya ya Igunga na wadau mbalimbali wa usafiri. Kulia ni mkuu wa wilaya ya Igunga John  Mwaipopo na kushoto ni kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Wilbroad Mtafungwa.
Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey  Mwanri (aliye na kofia ya kijani) akiwa eneo ambalo ajali ya basi la City Boy liligongana uso kwa uso na lori Jumatano usiku.

Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey  Mwanri akiliangalia basi la City Boy lililopata ajali ya kugonagana uso kwa uso na lori siku ya Jumatano usiku.


Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey  Mwanri (mwenye kofia ya kijani) na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo na ile ya wilaya ya Igunga wakiliangalia basi la City Boy lililopata ajali ya kugongana uso kwa uso na lori siku ya Jumatano usiku.


Mkuu wa mkoa wa Tabora, Aggrey  Mwanri akiwafariji majeruhi wa ajali ya basi la City Boy liliyogongana uso kwa uso na lori siku ya Jumatano usiku mara baada kutoka eneo ilipotokea ajali hiyo wilayani Igunga


Tiganya Vincent, Tabora

KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora na Wadau wa Usafiri wamependekeza uanzishwaji wa matumizi ya vitabu (log book) kwa magari ya mizigo ili kudhibiti madereva kusafiri mwendo mrefu bila kupumzika na hivyo kusababisha ajali kwa magari yao au kugongana uso kwa uso na mengine kutokana na uchovu.

Tamko hilo limetolewa jana wilayani Igunga na mkuu wa mkoa huo, Aggrey Mwanri mara baada ya kikao cha kujitathmini kwa ajili ya kuja na majibu ya kuondoa ajali za barabarani mkoani humo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema vitabu hivyo vitasaidia kuonesha muda aliotoka, mahali alipotoka na kama amesafiri muda mrefu atalazimisha apumzike ili kuepusha ajali.

Amesema malori yamekuwa yakisafiri mwendo mrefu bila hata dereva wake kupumzika jambo ambalo limesababisha magari hayo yapate ajali au wakati mwingine yawe chanzo kinachosabisha ajali katika magari ya abiria.

Mwanri amesema kwa kulitambua hilo wanaona wakati umefika kwa magari ya mizigo nayo kuwa na log book inayoonesha muda alioanza safari katika kituo chake cha kwanza na muda alipo baada ya kusimamishwa ili kuona kama kweli amezingatia matakwa ya kitaalamu na sheria ya kutokwenda kasi.

Amesema kitaalamu dereva anatakiwa aendeshe chombo cha moto kwa muda usiozidi saa nane lakini mara nyingi madereva wa malori wamekuwa wakiendesha magari yao hata zaidi ya muda huo jambo ambalo limekuwa kiwasababishia baadhi yao kuendesha huko wakisinzia na kupelelea magari yao kukosa mwelekeo na kupata ajali zinazoweza kuepukika.

Mwanri amesema ili kuepukana na hilo wadau wamependekeza wamiliki wa magari ya mizigo ya masafa marefu ni vema wawe na madereva wawili ili wasaidiane.

Mkuu huyo wa mkoa amesema hatua nyingine ambayo wameamua kuichukua ni pamoja na kuongeza askari na magari ya doria katika barabara kuu ya Igunga, Nzega kwenda Mwanza na Shinyanga.

Amebainisha kuwa hatua hiyo inalenga kupambana na madereva ambao nyakati za usiku wanakwenda mwendo mkali kwa sababu ya kujua kuwa tochi hazifanyi kazi wakati huo.

Mwanri ameongeza kuwa wadau wa usafiri wameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Tabora kuhakikisha wanaziba mashimo yaliyopo katika barabara kuu zote ili kuondoa uwezekano wa kuwa chanzo cha ajali za barabarani.

Aidha ametanabaisha kuwa wadau wamekuwabaliana kuwa ukaguzi wa madereva na magari katika barabara kuu zinazopita mkoani Tabora utakuwa unafanyika  kila siku ili kujihakikishia kama magari hayo yanao breki, taa zinazofanya kazi vizuri, matairi yako vizuri na dereva hajatumia kilevi.

Amesema hatua hiyo inalenga kujihakikishia kama chombo cha usafiri na dereva wake yuko katika hali nzuri.

Hivi karibuni Aprili 4, 2018, ilitokea ajali ambapo basi la abiria Kampuni ya City Boy lenye namba T 983 DCE liligongana uso kwa uso lori lenye namba T .486 ARB Mitsubishi Fuso wilayani Igunga na kusababisha watu 12 kufariki dunia papohpo na mmoja kufariki dunia akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Bugango, alikokimbizwa baada ya ajali hiyo.

Taarifa za awali zinaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa Fuso uliosababisha tairi kupasuka na gari kuhamia upande wa basi. Lori hilo lilikuwa na viazi ambavyo lilitoka navyo mkoani Njombe.

No comments:

Post a Comment