Thursday, 26 April 2018

Wafanyakazi JKCI watakiwa kuepuka rushwa


 Mwenyekiti wa  Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Profesa Mohamed Janabi akiongoza kikao cha baraza kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Msaidizi wa Baraza hilo, Renatha Miiruko.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza mada ya rushwa sehemu ya kazi iliyotolewa na Asseri  Mandari  kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) makao makuu wakati wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.


Brighton James - JKCI,

WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuepuka vitendo vya rushwa  ili waweze kutoa huduma bora za matibabu bila upendeleo.

Rai hiyo imetolewa leo na Asseri Mandari kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) makao makuu wakati akitoa mada ya rushwa sehemu ya kazi katika kikao cha Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa taasisi hiyo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mandari amesema katika maeneo mengi ya kutolea huduma za afya baadhi ya wagonjwa  wanashidwa au kuchelewa kupata huduma kutokana na mazingira ya rushwa kutawala.

“Ninawapongeza kwa huduma bora ya matibabu ya moyo mnayoyatoa kwa wananchi jambo muhimu ni kufanya kazi zenu kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma, kuwaheshimu wateja wenu bila ya kuwabagua kutokana na hali zao za maisha, kutumia lugha nzuri kwa wateja na kutunza siri ya kazi zenu”, amesisitiza Mandari.

Ameendelea kusema kuwa athari zinazotokana na vitendo vya rushwa ni pamoja na kushuka kwa pato la taifa kutokana na kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa, kudumaza mipango ya maendeleo na kuchochea umaskini kwa mtu mmoja mmoja au zaidi.

Athari zingine ni  wananchi kukosa imani na Serikali iliyopo madarakani, kushuka kwa kiwango cha uwajibikaji kazini, kukwamisha utoaji wa haki na kuongezeka kwa maovu.

Akitoa mada kuhusu kazi na uendeshaji wa majukumu ya baraza, Mkurugenzi msaidizi wa mabaraza kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,   Andrew Mwalwisi amesema baraza haliwezi kuwepo kama chama cha wafanyakazi hakipo, hivyo wajumbe wahakikishe wanawahamasisha wafanyakazi ili wajiunge na chama hicho.

Amesema wajumbe ni viongozi hivyo wanatakiwa kuwa na taarifa sahihi za maeneo yao ya kazi  na kushiriki kikamilifu katika vikao vya baraza la wafanyakazi kwa kutoa mapendekezo na ushauri wa kitu gani menejimenti ifanye ili kuboresha utoaji huduma na maslahi ya wafanyakazi na siyo kufanya uamuzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza,  Profesa Mohamed Janabi amewashukuru wajumbe wa baraza hilo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha huduma bora ya matibabu ya magonjwa ya moyo inatolewa  kwa wananchi.

“Mimi pamoja na Menejimenti yangu tutahakikisha kuwa maoni yote yaliyotolewa katika kikao hiki tunayafanyia kazi ili kuboresha ufanisi wa kazi katika taasisi yetu. Nanyi wajumbe mhakikishe kuwa yale yote yaliyofundishwa na kujadiliwa  katika kikao hiki mnakeenda kuyafanyia kazi.

“Boresheni utendaji wenu wa  kazi kwa kuhakikisha mnatoa huduma bora kwa wakati ikiwemo kuwahudumia vizuri wagonjwa na wateja wetu wengine, kuwahi kufika kazini na kuwepo eneo la kazi muda wote wa kazi kwa kufanya hivyo kutaongeza ufanisi wa kazi  na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi” amesema Profesa Janabi.

Katika kikao hicho mada mbalimbali zimejadiliwa ikiwa ni pamoja na rushwa sehemu ya kazi, uendeshaji wa majukumu ya Baraza na kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi kwa mwaka wa fedha 2017/18.

No comments:

Post a Comment