Monday, 9 April 2018

Wajawazito walivyo hatarini kupata kisukari kwa kula wanga kwa wingiInashauriwa mjamzito ale theluthi tu ya vyakula vya wanga

Claudia Kayombo

UGONJWA wa kisukari unajitokeza baada ya mwili kushindwa kudhibiti kiwango cha sukari (glucose), katika damu. Ukilinganisha na miaka ya nyuma, ugonjwa wa kisukari kwa sasa umekuwa tishio kubwa nchini na duniani kote.

Takwimu za Shirikisho la Kisukari Duniani (IDF), zinaonesha kuwa mtu mmoja kati ya kila watu 11 anakabiliwa na tatizo la ugonjwa wa kisukari. Wapo watu wazima milioni 425 duniani kote wanaosumbuliwa na maradhi hayo.

Hizo ni takwimu za ripoti ya mwaka uliopita ambapo zinabainisha kuwa mmoja kati ya wagonjwa wawili wa kisukari hafahamu kama ana ugua maradhi hayo.

Hiyo ina maanisha kwamba nusu ya wagonjwa wote milioni 425 wenye maradhi hayo hawajijui kama wanaugua. Takwimu nyingine zinaonesha kuwa karibu watu milioni 20 nchini Marekani wamekumbwa na maradhi ya kisukari.

Ugonjwa huu unawapata watu wa rika na jinsia zote huku kinamama wajawazito wakiwa katika wakati mgumu wa kudhibiti tatizo hilo hasa mimba inapokuwa na umri wa wiki 12 na wakati wanapokaribia kujifungua.

Dk. Cletus Kiwale anasema madhara ya kisukari wakati wa ujauzito yamegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani kwa mtoto ambaye bado hajazaliwa, kwa mama na mtoto baada ya kuzaliwa.

“Katika hatua za mwisho za mimba kisukari huleta madhara katika mfumo wa utendaji kazi wa kondo la nyuma kiasi kwamba mtoto aliye tumboni hushindwa kupata hewa ya kutosha hususan kunapokuwa na matatizo mengine kama kondo la nyuma kuachia, shinikizo la damu na uzazi kuchukua muda mrefu.

“Kiwango cha kuharibika mimba kinakuwa juu zaidi kwa wajawazito wenye kisukari kuliko wasio na tatizo hili,”  anabainisha.

Dk. Kiwale anasema watoto wanaozaliwa na kinamama wenye kisukari huzaliwa na uzito mkubwa kuliko kawaida na hivyo kusababisha uzazi kuwa na taabu kutokana na uwiano mbaya kati ya kichwa cha mtoto na ukubwa wa nyonga ya mama na kuzaa kwa njia ya upasuaji.

Aidha, ripoti ya mwaka jana inasema wajawazito hawako salama kutokana na maradhi hayo ambapo miongoni mwa wajawazito sita duniani, mmoja anakabiliwa na tatizo hilo na kwamba kuna watoto zaidi ya milioni moja wenye kisukari.
Wataalam wa masuala ya lishe nchini Uingereza wanasema vyakula vyenye wanga ama vya kuongeza nguvu na joto mwilini kama vile viazi, vinapaswa kuliwa theluthi moja tu na mama wajawazito ili kuepuka madhara mbalimbali ikiwemo kisukari.
Dk. Kammu Keneth anasema ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa maradhi sugu yanayoendelea kuathiri afya za mamilioni ya watu katika nchi nyingi duniani, ikiwemo Tanzania.
Anasema wagonjwa wa ugonjwa huu wamekuwa wakiongezeka haraka kiasi cha kuonekana kuwa ni janga la dunia.
“Pamoja na kuwa tatizo la kisukari linawakumba watu wa rika na jinsia tofauti, ila kupanda kwa kiwango cha kisukari kumeweza kuwa tatizo kubwa kwa wajawazito kiasi cha kuwasababishia matatizo mbalimbali wao na watoto wao walio tumboni,” anasema Dk. Keneth.
Anafafanua kuwa kisukari cha mimba kinawakumba asilimia tatu hadi tisa ya wanawake katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito. Tatizo hili linaweza kuwakumba hata wale ambao awali hawakuwahi kuugua ugonjwa huo.
Anatanabaisha kuwa asilimia 90 ya wanaokumbwa na tatizo hilo huweza kuondokana nalo baada tu ya kujifungua, ambapo linaathiri asilimia moja ya wanawake walio na umri wa chini ya miaka 20 na asilimia 30 ya walio na miaka 44.
Aidha, Dk. Keneth anasema utafiti umeonesha kuwa wanawake wenye kiwango kikubwa cha sukari kipindi cha ujauzito wapo katika hatari ya kujifungua watoto wenye kiwango kidogo cha sukari mwilini na wenye manjano.
“Kisukari cha mimba ni hatari na kama hakitatibika kinaweza kusababisha mtoto aliyeko tumboni kupoteza maisha,” anafafanua.
Anasema yapo mambo mengi yanayosababisha kisukari cha mimba ikiwemo uzito kupindukia, historia ya kuwa na kisukari cha mimba katika ujauzito uliopita, historia ya ugonjwa wa kisukari ukubwani katika familia na uvimbe katika ovari.
Pia kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa katika ujauzito uliopita, matumizi ya dawa aina ya glucocorticoids na beta blockers au antipsychotics wakati wa ujauzito, huongeza hatari ya tatizo hilo, kuwa na kiwango kikubwa cha presha ya damu wakati wa ujauzito. Wanawake wenye umri wa miaka 35 na zaidi wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata kisukari cha mimba.
Dk. Keneth ana shauri ni vema mjamzito mwenye kisukari ahudhurie kliniki mara kwa mara kulingana na maagizo ya daktari inaweza kusaidia kuondokana na tatizo hilo.
Mjamzito pia analo jukumu la kutunza afya yake kabla na baada ya kujifungua na ahakikisha anazingatia aina ya vyakula alivyoshauriwa kuvitumia pamoja na kufanya mazoezi.
Anafafanua kuwa wanawake wenye mpango wa kubeba mimba wakati tayari wanaugua kisukari wanatakiwa kupata virutubisho vya folate hadi kipindi cha wiki mbili wakati wa ujauzito kusudi waondokane na hatari ya kujifungua watoto wenye matatizo kwenye mfumo wa fahamu yanayofahamika kama ‘neural defects’.

No comments:

Post a Comment