Wednesday, 25 April 2018

Wanafunzi 15,000 kupata mafunzo usalama barabarani


Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu, Jenista Mhagama akikata utepe kuashiria uzinduzi wa miundombinu ya usalama barabarani katika shule za Msingi Mikumi na Mzimuni ikiwa ni mwendelezo wa mpango wa uboreshaji wa usalama barababarani kwa wanafunzi wa shule za msingi jijini Dar es Salaam ambao unaratibiwa na shirika la Amend kwa ufadhili wa Mfuko wakampuni ya Puma Energy na Mfuko wa Fia.


Suleiman Kasei

KAMPUNI ya Mafuta ya Puma Tanzania inatarajia kutoa mafunzo ya usalama barabarani kwa zaidi ya wanafunzi 15,000 kutoka shule za msingi 22 za mikoa ya Dar es Salaam na Ruvuma.

Hayo yamesemwa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Puma Tanzania, Philippe Corsaletti wakati akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Michoro ya Usalama Barabarani uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema katika mwaka huu mafunzo yatafanyika kwenye shule 22 za mikoa ya Dar es Salaam na Ruvuma na matarajio ni kuwafikia zaidi ya wanafunzi 15, 000.

Corsaletti amesema kampuni ya Puma imekuwa ikiindesha mpango huo tangu mwaka 2013 ambapo wametoa mafunzo kwa wanafunzi zaidi 60,000 wa shule 47 za mikoa mbalimbali.

“Puma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itatoa mafunzo ya ufahamu wa usalama barabarani ambayo yatahusu michoro ya ujumbe wenye usalama barabarani utaandikwa na kuchorwa kwenye kuta za shule za msingi na kutoa nafasi ya kushindana kiuchoraji kwa wanafunzi,” amesema.

Ameongeza elimu ya usalama barabarani imeweza kuwajengea uelewa wanafunzi wa matumizi ya barabara kwa usalama, hivyo kupunguza ajali.

“Tunawaangalia sana watoto wa shule za msingi kwani wao wanakabiliwa na hatari nyingi za barabarani. Hivyo kwa kuwafundisha usalama wa barabara tunawapa ufahamu na kuwajenga katika matumizi salama ya barabara. Na hiki ndicho kipaumbele chetu,” amesema.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, ASP Mbunja Matibu amesema jeshi hilo lipo pamoja na Puma kwa mchango wake wa kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi kwani wanawajenga katika msingi mzuri.

“Sina mengi ila nataka kusisitiza katika yale ambayo yamesemwa na wenzangu kuwa suala la usalama barabarani linahitaji ushiriki wa kila mdau kuanzia wanafunzi, walimu, wazazi na madereva ili kuepusha ajali ambazo zinatokea mara kwa mara.

Naye Simon Kalolo, Ofisa Miradi Taasisi ya Amend ambayo ni mdau wa usalama barabarani amesema wameamua kujikita katika masuala ya usalama barabarani ili kuhakikisha ajali zinaepukika.

Kalolo ameongeza kuwa taasisi yake inashirikiana na Puma kufikisha elimu katika shule mbalimbali ambazo zinakuwepo kwenye mpango hivyo dhana nzima ya uelimishaji inakamilika.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kisiwani, Floralist Wandioma, amesema amepokea mpango huo kwa mikono miwili ikizingatiwa kuwa shule yake ipo barabarani hivyo ni imani yake wanafunzi watanufaika.

Radhia Mfalingundi, Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Bunge amesema jitihada zinazofanywa na Puma zinapaswa kuungwa mkono kutokana na ukweli kuwa zinasaidia kuepusha ajali kwa watoto.

No comments:

Post a Comment