Saturday, 28 April 2018

Washauri kujenga utamaduni wa kufanya mazoeziWahudumu wa afya kwenye kambi maalum ya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo, wakiwafanyia upasuaji wagonjwa waliobainika kuwa na matatizo hayo.


Peter Simon

WATANZANIA wameshauriwa kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji pombe uliokithiri. Iwapo watazingatia hayo watajiepusha na magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yanaoua watu wengi zaidi duniani.

Ushauri huo umetolewa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka taasisi ya madaktari Afrika ya nchini Marekani, Mazen Albaghded wakati akizungumza na wanahabari kwenye kambi maalum ya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Dk. Albaghded amesema ulaji vyakula vyenye mafuta na bila kufanya mazoezi ambayo yangesaidia kuyeyusha mafuta hayo mwilini unaweza kusababisha kupata kirahisi ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo.

Wagonjwa wa kisukari  na wenye shinikizo la juu la damu  nao wanaweza kupata ugonjwa huo kirahisi.

“Mishipa ya damu inapozungukwa na mafuta  baadaye huweza kuziba  na hivyo damu kushindwa kwenda katika misuli ya moyo (myocardium) na kusababisha mtu kupata shambulio la moyo,” amesema.

Akizungumzia kuhusu kambi hiyo ya matibabu ya  siku nne, Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Tulizo Shemu amesema wagonjwa wanaotibiwa ni wale wanaohitaji matibabu ya kibingwa yenye uhitaji wa uchunguzi yakinifu.

Dk. Shemu amesema  kutumia mtambo wa Cathlab kwa njia ya kutoboa tundu dogo kwa mgonjwa wanaangalia kama mishipa ya moyo imeziba na ikiwa imeziba wanaizibua kwa kumuwekea mgonjwa  kifaa maalum kinachojulikana kwa jina la “stent” ambacho kinasaidia mshipa wa damu usizibe tena.

Katika kambi hiyo ambayo ilifanyika sanjari na mafunzo ya  kubadilishana ujuzi wa kazi, wagonjwa 23 wamefanyiwa vipimo na matibabu ambapo hali zao zinaendelea vizuri na wengine wameruhusiwa kurudi nyumbani.

No comments:

Post a Comment