Wednesday, 4 April 2018

Waziri acharuka aagiza ujenzi vivuko Kiteto kusimamishwaWaziri wa Tamisemi Selemani Jafo (kushoto) akikagua ujenzi wa vivuko katika barabara ya Namelock-Loltepes-Sunya yenye urefu wa Km 88 iliyopo katika wilaya ya Kiteto.

Mwandishi Wetu, Kiteto

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesimamisha ujenzi wa vivuko vyote kwenye barabara ya Namelock-Loltepes Sunya yenye urefu wa Km 88.1 inayojengwa katika wilaya ya Kiteto na mkandarasi, Deniko Constraction Ltd.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo mapema jana wakati wa ziara yake wilayani humo kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo amebaini mapungufu katika ujenzi wa vivuko zaidi ya 10 alivyovipitia.

Aidha kutokana na hali hiyo ameagiza mkandarasi aliyepewa kazi ya ujenzi wa barabara hiyo Deniko Construction sanjari na mhandisi mshauri Luptain Consult Ltd, Mhandisi Consulting Engineers pamoja na ACE Consultant kwenda ofisini kwake mara moja kutoa maelezo ya kina ya mapungufu hayo yaliyojitokeza katika ujenzi wa barabara hiyo.

“Ni mara ya tatu sasa nakuja kukagua barabara hii na kila mara nabaini changamoto tofauti sijui kuna tatizo gani nahitaji kusikia zaidi kutoka kwa wataalamu wa pande zote ili tutafute suluhisho kwa pamoja,”amesema Jaffo.

“Awali barabara hii iligawanywa kwa wakandarasi wajenzi wawili ambaye ni Deniko alikuwa anajenga upande mmoja wenye Km 44 na Km nyingine 44 alipewa Maginga Construction ambaye alishindwa kazi hiyo ndipo nilipoagiza taratibu zifuatwe ili kuvunja mkataba wa awali na kazi ile apewe Mkandarasi mwingine.

“Kazi hii aliongezewa Deniko Construction ambaye kwa sasa ndiye anayejengwa barabara hii yote yenye Km 88. Hapo awali kazi yake ilionekana nzuri sana na ya kuridhisha lakini baada ya mvua za msimu huu mapungufu makubwa yamebainika hasa katika vivuko vyote vilivyojengwa haviendani na mahitaji ya barabara hii,” amesema Jaffo.

Naye Kaimu Meneja wa Tarura wilaya ya Kiteto, Elias Paul amesema tatizo lililobainika katika ujenzi wa vivuko hivyo haviendani na wingi wa maji  yanayopita na vipenyo vya vivuko ni vidogo hivyo havina uwezo wa kuhimili na takataka nyingine zinazotakiwa kupita hapo ni rahisi sana kuziba hata kivuko chote kubebwa na maji ndani ya kipindi kifupi.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Nmelock – Loltepes – Sunya unatekelezwa na Serikali kupitia fedha za wafadhili kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID) chini ya mpango wa (Feed for future) unaotekelezwa katika wilaya Nne nchini ambazo ni Kilombero, Mvomero, Kongwa na Kiteto.

No comments:

Post a Comment