Friday, 20 April 2018

Waziri mkuu kuzindua mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka Tanzania kesho Jumamosi


Mathias Canal, NFRA-Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa Aprili 21, 2018 (kesho) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za uwekaji jiwe la msingi mradi wa kuongeza uwezo wa uhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Tukio hilo linatarajiwa kujiri katika dhifa itakayofanyika kwenye viwanja vya ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula zilizopo Mtaa wa Kizota eneo la Viwanda Mjini Dodoma.

Mradi huo utagharimu Dola za Marekani milioni 55, ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha dola milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, mikataba ya ujenzi ilianza kutekelezwa Desemba 9, 2017 ambapo mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o) huku msimamizi wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na kaimu ofisa mtendaji mkuu wa NFRA, Vumilia Zikankuba imesema mradi huo utahusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa, ujenzi wa ofisi na kutekelezwa katika maeneo manane ambayo ni Babati- Manyara, Dodoma, Makambako-Njombe, Mbozi-Songwe, Shinyanga, Songea-Ruvuma, Sumbawanga-Rukwa na Mpanda-Katavi.  

Kupatikana mradi huo nchini ni jitihada za Serikali ambazo zitapelekea ukuaji uchumi nchini na kuchangia kuiwezesha Tanzania ya viwanda ambapo kutawezesha maghala ya wakala kuhifadhi akiba ya chakula ambayo itaendana na mahitaji halisi ya dharura kulinganisha na ongezeko la watu nchini.

Hifadhi ya chakula inayohitajika kukidhi mahitaji ya dharula kwa miezi mitatu ni zaidi ya tani 500,000 ukilinganisha na tani 150,000 iliyokuwa inahitajika miaka ya 2008 Wakala ulipoanzishwa.

Aidha, Zikankuba amesema technolojia itakayotumika katika ujenzi wa vihenge vya kisasa, itawezesha Wakala kupunguza gharama za uendeshaji; kuhifadhi chakula kwa muda mrefu zaidi; kupunguza upotevu wa zao la mahindi baada ya kuvuna (posthaverst loss), kuongeza soko la mahindi nchini na kuimarisha usalama wa nafaka inayohifadhiwa kwa kudhibiti sumukuvu kwa mahindi yaliyohifadhiwa. 

Jitihada hizi zinalenga kuimarisha uwezo wa taifa katika kuimarisha usalama wa chakula nchini.

No comments:

Post a Comment