Sunday, 29 April 2018

Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani azindua kiwanda cha kutengeneza mita za luku Dar es Salaam

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani sanjari na wabia wa kampuni ya Baobao Energy System akikata utepe kuashiria kufunguliwa rasmi  kiwanda hicho.


Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani akizungumza na baadhi wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali na wafanyakazi wa kiwanda cha Baobao Energy System Tanzania wakati wa kuzinduliwa kwake ambacho kitajihusisha na utengenezaji wa mita la Luku, tukio lililofanyika jana Dar es Salaam.


Meneja Mkuu wa  kampuni ya Baobao Energy System Mhandisi Hashim Ibrahim akizungumzia kiwanda hicho kitakachokuwa kinatengeneza mita za LUKU hapahapa nchini wakati wa uzinduzi uliofanywa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani.

Mkurugenzi wa Mkuu wa Mauzo wa EDMI Lam Wee Chee akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha Baobao Energy System Dar es Salaam jana.


Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani akifunua kitambaa kilichofunikwa mahali lilipo jiwe la msingi la kiwanda hiyo kuashiria uzinduzi wake.


Meneja Mkuu wa Baobao Energy System, Hashim Ibrahim akimueleza jambo Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani alipokua akikagua chumba kinachotumika kutengeneza mita za LUKU wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho.


Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani akikagua mitambo inayotumika wakati wa utengenezeaji wa mita za LUKU  jana Dar es Salaam.


Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani akipatiwa maelezo na wafanyakazi wa kiwanda hicho namna wanavyoweza kutengeneza mita za LUKU zenye ubora. (PICHA ZOTE NA ZAINAB NYAMKA).

Leandra Gabriel

KATIKA kuelekea uchumi wa kati wa viwanda kampuni ya Baobao Energy Systems Tanzania (BEST) imefungua kiwanda cha kutengeneza mita za umeme za luku na hii ni kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda na kufikia uchumi wa kati kufikia 2025.

Akizungumza katika uzinduzi huo mgeni rasmi ambaye pia Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amesema amefurahishwa na kufarijika kwa kupata mwaliko wa kuzindua kiwanda hicho kwani mita za luku zinategemewa na wadau wengi nchini na amewapongeza na kuwataka Tanesco kujipanga katika kukabiliana na changamoto za kukidhi mahitaji ya kutoa huduma za umeme kwa wananchi.

Aidha Dk. Kalemani ameeleza kuwa Julai Mosi mwaka huu hakuna mita za luku zitakazoagizwa kutoka nje na hii ni baada ya kufanya tathimini kwa miezi mitatu na kujiridhisha na uzalishwaji wa mita hizo hapa nchini na kuanzia Mei mwaka huu mita za luku zitanunuliwa kutoka Baobab.

Pia Dk. Kalemani amewataka wamiliki wa kiwanda hicho kuzingatia uharaka wa utengenezaji, wingi wa mita hizo, ubora na upatikanaji wake kirahisi. Ameelezea umuhimu wa mita hizo ikiwa ni pamoja na matengenezo pindi zinapoharibika, gharama nafuu na uharaka tofauti na zile zinazoagizwa nje na amewataka Tanesco kuunganisha umeme kwa siku zisizozidi 7.

Mwakilishi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Aristides Mbwasi amewapongeza wamiliki na kiwanda hicho na kuahidi ushirikiano pale watakapohitaji kwani kwa sasa taifa lipo katika malengo ya kuijenga Tanzania mpya kama Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoazimia.

Naye Meneja mkuu wa kampuni ya Baobab Energy Systems Tanzania, Mhandisi Hashim Ibrahim amemshukuru waziri wa nishati kwa kuja kufungua kiwanda hicho na kueleza kuwa kampuni hiyo ni ya ubia baina ya kampuni ya Comfix Engineering Ltd ya Tanzania inayomiliki hisa kwa asilimia 51 na hii ni kwa kutoa mchango wa fedha, majengo, rasilimali watu na fedha na kampuni ya EDMI ya nchini Singapore inayomiliki hisa kwa asilimia 49 na kuchangia mtaji kupitia mitambo na teknolojia kwa ujumla.

Mhandisi Hashim ameeleza kuwa hawaogopi ushindani na kampuni za nje ila tatizo lao ni pale kampuni hizo zinapopewa unafuu wa gharama na uzalishaji na ameiomba serikali kutoa ushirikiano ili kuweza kujenga Tanzania ya viwanda na ameeleza kuwa wanampango wa kutengeneza mita za gesi na maji hapo baadaye.

Kuhusu uzalishaji wa mita katika kiwanda hicho Hashim amesema mita zitakazotengenezwa na kuuzwa nje na ndani ya nchi zitaliongezea taifa mapato yanayotarajiwa kufikia sh. bilioni 97 kwa mwaka.

Pia Mkurugenzi mkuu mauzo wa Kampuni ya EDMI ya nchini Singapore, Lam Wee Chee amesema kwa miaka 10 kampuni ya EDMI imefanya kazi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hususan ya kusambaza mita hizo na zaidi ya mita 100,000 zimenunuliwa na Tanesco kutoka EDMI na kwa sasa watawapa mfumo utakaowasaidia kusoma taarifa zote na kudhibiti wizi wa umeme.

No comments:

Post a Comment