Sunday, 22 April 2018

WB kushirikiana na serikali kukomesha mafuriko bonde la Msimbazi


Dk. Philip Mpango 
Mwandishi Wetu
BENKI ya Dunia (WB), itashirikiana na Serikali ya Tanzania kukabiliana na athari za mafuriko zinazosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha kila mwaka katika jiji la Dar es Salaam hasa eneo la Jangwani.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango wakati akizungumza na ujumbe wa Benki ya Dunia katika mikutano ya kipupwe inayoendelea mjini Washington DC.
Dk. Mpango amesema WB imekubali kusaidia kukabiliana na mafuriko katika bonde la mto Msimbazi hasa katika eneo la kutoka Magomeni Mapipa kwenda Faya na tayari imeanza mchakato wa kutafiti eneo la Jangwani ili kuweza kuangalia namna nzuri ya kugharamia uboreshaji wa mifereji katika bonde la mto Msimbazi.
“Tumewaeleza changamoto ambayo imekuwa inajirudia kila mara na kusababisha upotevu wa maisha ya watu, kusababisha kufungwa kwa barabara, watu kushindwa kwenda kazini na wanafunzi kushindwa kwenda shule, hivyo wameonesha nia ya kumaliza kero hii kwa wananchi,” amesema Dk. Mpango.
Ameongeza kuwa baada ya timu ya WB kumaliza kufanya kazi yao kwa kushirikiana na manispaa za jiji la Dar es Salaam, Serikali inaamini njia ya kudumu itapatikana na kuondokana na tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment