Saturday, 7 April 2018

Zuma awa ngangari mbele ya mashtaka ya rushwa


 Jocob Zuma akiwa mahakamani

RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amefikishwa kizimbani katika mahakama iliyofurika watu jana Ijumaa akikabiliwa na mashtaka ya rushwa na aliibuka mkaidi, akiyataja mashtaka hayo kuwa yaliyochochewa kisiasa.

Zuma mwenye umri wa miaka 75, alionekana mtulivu wakati wa usikilizaji wa kwanza wa kesi hiyo uliodumu kwa dakika 15 tu, iliyoahirishwa hafi Juni 8 mwaka huu.

Jaji Themba Sishi ameahirisha kesi hiyo, baada ya kuwasilikiza mawakili wa pande zote waliothibitisha kuwa Zuma atakata rufaa kupinga uamuzi wa kumshitaki. Polisi iliimarisha usalama nje ya jengo la mahakama, lakini tukio hilo limepita kwa amani.

Wakati mapambano ya muda mrefu yanatarajiwa, tukio la Zuma kusimama mbele ya majaji ikiwa ni miezi miwili baada ya kujiuzulu wadhifa wake, lilikuwa ushindi kwa wanasiasa wa upinzani na wanaharakati waliopigana kwa miaka kadhaa kumwajibisha.

Mashitaka 16 ya hongo, udanganyifu na utakatishaji fedha yalirejeshwa hivi karibuni baada ya kutupiliwa mbali karibu muongo mmoja uliopita. Yanahusiana na mkataba wa silaha katika miaka ya 1990, wakati Zuma alipokuwa naibu rais.

Zuma anashtumiwa kwa kuchukuwa hongo kutoka kampuni ya Ufaransa inayotengeneza silaha ya Thales, katika mkataba wa mamilioni ya dola, wakati alipokuwa waziri wa uchumi na wakati huo makamu wa rais wa chama tawala cha Afrika Kusini, ANC.

Kampuni ya Thales, ambayo iliiuzia Afrika Kusini meli za kivita kama sehemu ya mkataba huo, pia anakabiliwa na mashtaka ya rushwa na mwakilishi wa kampuni hiyo alihudhuria mahakamani pamoja na Zuma.

Zuma anadaiwa kuchukuwa kinyume na sheria randi milioni 4.7, sawa na Euro 280,000 kwa kiwango cha sasa cha ubadilishaji fedha kutoka malipo 783 yaliyoshughulikiwa na Schabir Shaik, mfanyabiashara aliyekuwa mshauri wake wa kibiashara.

Shaik alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani mwaka 2005 kwa tuhuma sawa na hizo, lakini uchunguzi uliookolewa sana mwaka 2016, ulimuondolea lawama Zuma.

Zuma ambaye aliingia madarakani mwaka 2009 baada ya kuondolewa mashtaka, anakanusha kutenda kosa lolote, na anadai kuwa tume ya uchunguzi ilithibitisha kuwa hakuna ushahidi wowote kwamba fedha zilizopokelewa na yeyote miongoni mwa washauri zililipwa kwa ofisa yeyote.

Nje ya jengo la mahakama, Zuma aliimba na kucheza jukwani mbele ya kundi kubwa la wafuasi wake, wengi wao wakiwa wamevalia nguo za rangi za chama cha ANC. Aliwambia wafuasi kuwa yeye ni mhanga wa visasi vya kisiasa.

Aliongeza kuwa amekuwa akipigania haki za kiuchumi za raia weusi wa Afrika Kusini walio wengi tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi wa weupe wachache mwaka 1994.

Ujumbe huo unavuma miongoni mwa watu wengi wanaochukia ukweli kwamba sehemu kubwa ya uchumi inaendelea kuwa mikononi mwa wazungu wachache licha ya kuja kwa demokrasia.

"Mtu anapotuhumiwa kwa uhalifu, hilo halimaanishi kwamba wamekutwa na hatia. Mtu huyo bado ana haki kama mtu mwingine yeyote," alisema Zuma.

Mwezi uliopita mwendesha mashtaka mkuu wa Afrika Kusini Shaum Abrahams aliyepachikwa jina la utani la "Shaun Kondo" kutokana na utiifu wake kwa Zuma wakati wa urais wake aliagiza Zuma ashtakiwe kwa udanganyifu, rushwa na utakatishaji fedha.

Chama cha ANC kilimlaazimisha Zuma kuachia madaraka mwezi Februari, baada ya sehemu kubwa na changamoto za kisheria zilizokuwa zikiongezeka dhidi yake pamoja na kashfa kadhaa za rushwa, na chama hicho kimejitenga na kiongozi wake huyo wa zamani.

Mrithi wa Zuma Cyril Ramaphosa ameapa kupambana dhidi ya rushwa serikalini, ambayo alikiri kuwa ni tatizo kubwa.
Chanzo DW

No comments:

Post a Comment