Tuesday, 1 May 2018

ACT Wazalendo Dar yajipanga kunyakua viti 20 serikali za mitaaClaudia Kayombo

CHAMA cha ACT Wazalendo, mkoa wa Dar es Salaam kinajipanga kunyakua viti zaidi ya 20 katika uchaguzi wa wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoa wa Dar es Salaam, Salimu Sudi ametoa kauli hiyo juzi Dar es Salaam katika mkutano wa ndani uliofanyika Temeke ili kuwapokea na kuwapa kadi wanachama wapya 118 waliojiunga na chama hicho kati ya Januari na Aprili mwaka huu.

Sudi amesema katika mkoa wa Dar es Salaam hakuna mtaa, kata na hata jimbo linaloongozwa na chama hicho na kwamba wanatekeleza mikakati mbalimbali ya kuwapata wenyeviti wa mitaa zaidi ya 20, madiwani na wabunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Amesema mikakati wanayofanya ni pamoja na kuteua wanachama wenye ushawishi na uwezo wa kuongoza bila kujali wamedumu muda gani ndani ya chama hicho sanjari na kujenga matawi ya chama katika maeneo mbalimbali ya manispaa za jiji hilo.

Mwenyekiti huyo amesema pia wanaanzisha ligi ya mpira wa miguu wa vijana na wanawake katika majimbo yote ya mkoa huo ili kuamsha hamasa kwa wanachama na wasio wanachama kujiunga nacho ili kuongeza idadi yao.

Amebainisha kuwa hadi sasa mipira na jezi vimeshanunuliwa na kwamba ligi hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi mapema mwezi huu wa Mei.

Sanjari na hayo, Sudi amesema ACT Wazalendo kinachozingatia na kujali utu, uwazi na uadilifu kinakusudia kuwatumia wananchi wote bila ubaguzi.

Ametoa mwito kwa Watanzania kujiunga nacho kwa kuwa hakina sera za ubaguzi bali kinajali utu wa kila mtu.

No comments:

Post a Comment