Saturday, 26 May 2018

Atakayethubutu kuvamia hifadhi ya Uzigua kukiona cha moto- Ndikilo


Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo (mwenye suti nyeusi) akiwa ndani ya msitu wa hifadhi wa Taifa Uzigua, kushoto ni mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaj Majid Mwanga.


Ofisa msaidizi wa misitu Bagamoyo, Jonathan Mpangala, akionesha mipaka ambayo imewekwa katika msitu wa hifadhi wa Taifa Uzigua, wakati mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo (wa katikati mwenye suti) alipotembelea msitu huo.

Bango linaloonesha msitu wa hifadhi ya Taifa wa Uzigua (PICHA ZOTE NA MWAMVUA MWINYI)

Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo

MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo amewaonya wote wanaokusudia kuvamia msitu wa hifadhi Uzigua kuwa wakikamatwa watakiona cha moto.

Aidha, ameutaka wakala wa misitu kanda ya Mashariki na wilaya nzima ya Bagamoyo kuendelea kufanya doria ili kudhibiti uvamizi uliokuwepo kipindi cha nyuma.

Akizungumza akiwa hifadhini humo alipokwenda kujiridhisha kama umeanza kurejesha uoto wake wa asili, Ndikilo amewaasa wananchi wakiwemo wafugaji kuheshimu mipaka iliyopo na kuulinda msitu huo.

Amesema mwaka mmoja uliopita serikali ilifanya oparesheni kali ambapo ilifanikiwa kuziondoa kaya zaidi ya 500 na maboma ya mifugo ya ng’ombe ndani ya hifadhi hiyo.

Hata hivyo, Ndikilo amesema, kwasasa kumewekwa vigingi vidogo na vikubwa kama mipaka vinavyoonesha upande wa msitu na upande wa wananchi hivyo wasiendelee kupita katika njia zinazoingia msituni kwani wakikamatwa sheria itafuata mkondo wake.

“Kuna watu walivamia na wengine kuanza kuishi, kuvuna mbao, kukata miti kwa ajili ya mkaa, kuni, kufuga ng’ombe, kilimo, uchimbaji wa madini na kusababisha athari kubwa kwa msitu. 

“Msitu huu ni eneo la maji yanayoingia mto Wami, tuliondoa watu wote na leo nimepita nimejiridhisha nimeona wanyama wameanza kurejea, wanyama wana njia zao hususan tembo, tumeona wameanza kupita kwenye mapito yao kuelekea Wamimbiki, Saadan.

“Miti nayo imeanza kuota hivyo uoto wa asili unajirudia kama zamani, jamii ikiiona inafukuzwa katika misitu ijue ni kwa ajili ya manufaa yao,”amesema Ndikilo.

No comments:

Post a Comment