Wednesday, 9 May 2018

Bilioni 3 kujengea hospitali za wilaya Itilima, Busega


Josephat Kandege

Claudia Kayombo

SERIKALI imetenga sh. bilioni 3 kwa ajili kuanza ujenzi wa hospitali za wilaya ya Itilima na Busega katika mkoa wa Simiyu.

Waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege ametoa kauli hiyo leo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum, Esta Midimu.

Katika swali lake, Esta alihoji kuwa wilaya mpya za Busega na Itilima hazina hospitali za wilaya. Ni lini serikali itajenga hospitali za wilaya hizo?

“Ni kweli wilaya hizi hazina hospitali za wilaya, wananchi wanapata huduma za afya kupitia zahanati 45 na vituo vya afya 7, kati ya hivyo zahanati 27 na vituo vya afya vitatu vipo wilaya ya Itilima na zahanati 18 na vituo vya afya vinne vipo Busega.

Serikali itapeleka sh. bilioni 1.5 kwa kila wilaya (Itilima na Busega) kwa ajili ya kuanza ujenzi wake. Kupitia mpango wa maboresho ya huduma za afya serikali imepeleka sh. bilioni 1.2 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika vituo vya afya vya wilaya hizo.,”amesema Kandege.

Wakati huo huo, naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile amesema miongoni mwa magari ya wagonjwa yaliyoagizwa na serikali yatakapofika, hospitali ya mkoa wa Simiyu itakuwa miongoni mwa zile zitakazonufaika.

Dk. Ndugulile ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Esta Mdimu aliyetaka kufahamu ni lini serikali itapeleka gari la wagonjwa katika hospitali hiyo ambayo haina hata moja ambalo litasaidia kuwapeleka katika hospitali ya rufaa Bugando wagonjwa watakaopewa rufaa.

No comments:

Post a Comment